Na. Mwandishi Wetu.
Jeshi la Polisi.Jeshi la Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini katika kuhakikisha linaboresha huduma bora kwa Wananchi limeendelea kuwatambua na kuwapongeza Askari wa Jeshi hilo wanaofanya kazi vizuri zaidi ya kuhudumia wananchi sambamba na kuzuia uhalifu.
Akitoa vyeti vya Pongezi kwa Askari hao leo Machi 01, 2024 katika bwalo la maafisa wa Polisi Arusha, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Utawala na Uchumi Bwana Daniel Luloku pamoja na kuwapongeza Askari waliofanya vizuri zaidi amewataka kwenda kufanya kazi kwa nidhamu na kwa weledi mkubwa ilikuhakikisha raia na mali zao wanabaki kuwa salama wakati wote.
Bwana Daniel amewataka Askari wengine kuiga mfano mzuri kutoka kwa Askari waliopata vyeti vya sifa na zawadi lakini pia kuongeza juhudi katika utendaji wao wa kazi za kila siku.
Aidha amebainisha kuwa amefurahishwa na namna ambavyo Jeshi hilo linatumia mbinu ya kubaini na kuzuia matukio ya uhalifu katika jamii kabla ya kutokea huku akitoa wito kwa Jeshi hilo kuendelea kuimarisha mahusiano mazuri na sekta binafsi.
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Simon Pasua amesema Jeshi hilo limekua na utaratibu wa kuwatambua na kuwapongeza Askari wanaofanya kazi vizuri zaidi kila mwaka pamoja na kuwatambua wadau walioshirikiana na Jeshi hilo.
SACP Pasua ameongeza kuwa Jeshi hilo litaendelea kuwatambua na kuwapongeza Maafisa, Wakaguzi na Askari watakaofanya kazi vizuri ya kutoa huduma bora ikiwa ni pamoja na kubaini na kutanzua uhalifu hususani ya Wizi wa Mifugo.
Naye Mkaguzi Msaidizi wa Polisi A/INSP Julius Makrk kwa niaba ya Askari waliopata vyeti vya sifa na zawadi pamoja na kushukuru Jeshi hilo kwa kutambua kwa utendaji wao wa kazi, amebainisha kuwa zawadi hiyo imetokana na ushirikiano mzuritoka kwa Askari wengine katika kuzuia uhalifu huku akisema zawadi hiyo itaongeza ufanisi katika utendaji wao wa kazi