Na Sixmund Begashe – Ngara
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Benedict Wakulyamba ametembelea eneo la Bonde la Nyati kujionea namna baadhi ya wafugaji wa Ng’ombe wanavyoathiri shughuli za Uhifadhi kwa kuingiza mifugo ndani ya Hifadhi ya Taifa Burigichato eneo la Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera.
Akiwa kwenye Hifadhi hiyo, CP Wakulyamba amejionea namna baadhi ya wafugaji walivyoweka uzio mita takribani kumi kutoka kwenye mpaka wa hifadhi kinyume cha sheria na kuathiri shughuli za Uhifadhi wa Maliasili katika Hifadhi ya Burigichato inayopatikana katika Mkoa wa Kagera na Geita.
“Uzio huu umejengwa ndani ya mita 500 zinazozuiwa na sheria kufanyika kwa shughili zozote za kibinadamu ni bayana kabisa kuna uwepo wa mazingira ya wananchi hawa kutumia maeneo ya Hifadhi kwa malisho isivyo halali”. Alieleza Kamishna Wakulyamba
Aidha CP Wakulyamba akiwa ameambatana na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi TANAPA Ignus Gara na Maafisa wengine wa TANAPA, ndani ya Bonde la Nyati, amekutana na kuzungumza na jamii ya wafugaji walio jenga uzio kinyume cha sheria, na kuwataka wafugaji hao kufuata sheria za uhifadhi ili kuepuka mivutano na Wahifadhi na kutowasumbua Wanyamapori hususani Tembo ambao wakipata kadhia kama hizo hukimbilia kwenye makazi ya wananchi.