Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya utumishi wa mahakama Prof.Ibrahim Juma akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Majaji Wafawidhi kutoka mikoa yote nchini.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya utumishi wa mahakama Prof.Elisante Ole Gabriel akizungumza katika mafunzo hayo yanayoendelea mkoani Arusha.
Pichani ni baadhi ya majaji Wafawidhi kutoka mikoa mbalimbali wakiwa katika mafunzo hayo.
………..
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha .JAJI Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya utumishi wa Mahakama Prof.Ibrahim Hamis Juma amewataka Majaji Wafawidhi nchini kuwachukulia hatua za kisheria mawakili wote ambao wamekuwa hawawatendei haki wananchi na kupelekea kuendelea kuwepo kwa malalamiko kutokana na kutoridhika na maamuzi yanayotolewa.
Ameyasema hayo leo mkoani Arusha wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Majaji Wafawidhi ili waweze kuwa wakufunzi wa kamati za maadili za Maafisa Mahakama za mkoa na wilaya yaliyoandaliwa na Tume ya Utumishi ya Mahakama .
Amesema kuwa ,mafunzo hayo ni muhimu sana kwa Majaji Wafawidhi sio tu kwa ajili ya kutekeleza jukumu la kuwafundisha Wajumbe wa Kamati za Maadili ngazi ya Mkoa na Wilaya,kwani wao ni walezi katika maswala ya nidhamu na maadili kwa watumishi.
Aidha amesema kuwa ,lengo la mafunzo hayo ni kuwapatia mafunzo kama Wakufunzi (ToTs) ili
kuwajengea uwezo wa kutoa mafunzo yanayofanana (equal standard) kwa Wajumbe wa Kamati za Maadili za Maafisa Mahakama za Mkoa na Wilaya katika Mkoa mlipo,Kutoa mafunzo kuhusu Kanuni na Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili za Maafisa Mahakama za mwaka, 2023 ,pamoja na mafunzo ya mara kwa mara yatakayotolewa na Majaji Wafawidhi yatazisaidia Kamati za Maadili za Mkoa na Wilaya ziweze kutumia Miongozo waliyopewa na Tume pasipo kuingilia uhuru wa Kikatiba wa Hakimu kusikiliza mashauri na kufikia maamuzi yao bila kuingiliwa au kutiwa woga, ushawishi au shinikizo kutoka Kamati za Maadili
Jaji Prof .Juma amesema kuwa ,wataweza kubadilishana uzoefu kuhusu makosa mbalimbali yanayotendeka ambayo yanakinzana na Kanuni za Mwenendo na Maadili ya Maafisa Mahakama za 2020,huku mada zitakazotolewa ikiwa ni Tume ya Utumishi wa Mahakama na Majukumu yake,Mgawanyo wa Madaraka na Uhuru wa Mahakama,Kanuni za Uendeshaji wa Kamati za Maadili za Afisa Mahakama za Mkoa na Wilaya,Kanuni za Madili za Maafisa Mahakama,Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama,Mbali na kwamba ipo Sheria ya Usimamizi wa Mahakama ya mwaka 2011 na Kanuni za Jumla za Usimamizi wa Mahakama za Mwaka 2021, Tume iliandaa Kanuni za Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mkoa na Wilaya za Mwaka 2023 na Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama.
“Watumiaji wa huduma za Mahakama lazima nao wawe waadilifu Uadilifu wa Mahakimu, Wasajili, Majaji hauwezi kufikia asilimia 99 tunayotafuta, endapo wadaawa na wananchi katika mnyororo wa Haki uadilifu wao utakuwa ni pungufu,kwa mfano mdaawa ana kesi inaendelea Mahakamani, au anayo nafasi ya kukata rufani- lakini ataandika barua kwa Mhe. Rais, Jaji Mkuu au Jaji Kiongozi. Kwamba “waingilie kati”. Maombi ya aina hii hatarishi kwa uhuru wa Mahakama.”amesema Jaji Mkuu.
Amefafanua kuwa,baadhi ya vitendo vinavyolalamikiwa dhidi ya Mawakili, ambazo zipo kwenye kumbukumbu ya majalada ya Advocates Committee ni pamoja na Wakili kufanya fujo Mahakamani, kutoa lugha isiyofaa,Kutotunza kwa makusudi siri za wateja ,Kutafuna fedha za mteja, kwa mfano malipo ya mirathi, au malipo kwa aliyeshinda hukumu na tuzo kulipwa kupitia akaunti ya Wakili; Kugushi nyaraka .
Naye Mtendaji Mkuu wa mahakama ya Tanzania na katibu wa Tume ya utumishi wa mahakama Prof.Elisante Ole Gabriel amesema kuwa mafunzo hayo ya siku mbili yatawasaidia kuwa wakufunzi katika maswala ya maadili na kuweza kutekeleza jukumu la kuwafundisha wajumbe wa kamati hizo.
Aidha amesema kuwa ,swala la uadilifu kwa majaji ni swala kubwa na linapaswa kuzingatiwa kwa kiwango cha hali ya juu huku wakihakikisha utoaji haki kwa wananchi unazingatiwa pande zote mbili.
Kwa upande wake Jaji mfawidhi wa mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma ,Juliana Masabo amesema kuwa mafunzo hayo yanawaandaa waweze kuwa wawezeshaji wazuri katika kutoa elimu kuhusu maswala mbalimbali katika kamati za maadili za maafisa mahakama za mkoa na wilaya mkoani Arusha.