WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuwatumikia Watanzania kwa kuhakikisha fedha za maendeleo zinafika kwenye sekta zote katika kila eneo nchini.
“Rais wetu Dkt. Samia anatekeleza miradi mbalimbali ya maeneo katika sekta zote za maendeleo kuanzia ngazi ya Taifa hadi vijijini ili kuhakikisha maisha ya Watanzania yanakuwa bora.”
Akiwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi ya Bwai, eneo la Bwai Kumsoma, Waziri Mkuu aliwaelezea wananchi hao hatua mbalimbali ambazo Serikali imechukua kwenye sekta za maji, elimu, umeme na barabara.
Akijibu hoja ya Mbunge wa Viti maalum, Agnes Marwa kuhusu mikopo umiza kwa wajasiriamali wa kata hiyo, Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi hao kuwa mikopo iliyokuwa inatolewa na Halmashauri ya asilimia 10, itarudishwa hivi karibuni baada ya taratibu kukamilika na hiyo mikopo umiza haitakuwepo.
Awali, Agnes Marwa alisema wako wajasiriamali wadogo wengi ambao wanaumizwa na mikopo umiza akaomba Serikali iingilie kati ili waweze kupata mikopo sahihi.
Kuhusu hoja ya Halmashauri hiyo kuwa na shule ya sekondari ya wasichana ya bweni ambayo ilitolewa na Mbunge wa Viti maalum, Esther Matiko, Waziri Mkuu alisema uamuzi wa kuwa na shule ya aina hiyo bado uko kwenye ngazi ya Halmashauri na kwenye Baraza la Madiwani.
Awali, Esther Matiko aliiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuwajengea sekondari ya bweni ya wasichana katika Halmashauri hiyo kwa sababu ya umbali uliopo. “Jiografia ya Halmashauri hii ni kubwa sana, ziko sekondari zaidi ya 20. Tunaomba sekondari ya wasichana ya bweni ili wapate muda mzuri wa kusoma tuweze kuwapata akina Samia wengi,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuokoa Bi. Maria Abihudi aliyeomba arudishiwe nyumba yake kwa kuchangia sh. milioni 2.8 za papo hapo ili zimsaidie kulipa deni lililosababisha nyumba yake iuzwe kwa mnada kwa amri ya Baraza la Kata la Ardhi.
Waziri Mkuu Mkuu amesisitiza kuwa ni lazima waheshimu maamuzi yaliyotolewa na vyombo vya kisheria wakati wakishughulikia suala la kumrejeshea nyumba mama huyo.
Amemkabidhi Mkuu wa Mkoa huo, Saidi Mtanda, sh. milioni 2.5 na kumpatia mama huyo sh. 300,000 ambayo ilikuwa ni ziada ya changizo huku akimtaka Mkuu huyo wa mkoa kwanza ajiridhishe na utaratibu mzima.
Kati ya fedha hizo, sh. 500,000 zitaenda kwa mnunuzi ambaye tayari alitoa malipo ya awali kwenye Baraza la Ardhi la Kata lakini baada ya kuombwa na Mkuu wa Mkoa, amhurumie mama huyo, alikubali kutoendelea na nia yake ya kununua nyumba lakini akataka arudishiwe hela yake na huyo mama hakuwa nayo.
Aidha, shilingi milioni mbili zitaenda kwenye Baraza la Kata ambalo lilitoa maamuzi ya kuuza nyumba ya mama huyo ili kufidia gharama za kesi baada ya kushindwa kuhudhuria kwenye baraza licha ya kuitwa mara kadhaa.
Mama huyo alifikishwa kwenye baraza hilo na jirani yake ambaye walikuwa wanagombea mpaka. Alidai kuwa alishindwa kuitikia miito ya Baraza kwa vile alikuwa mjamzito na alienda kujifungua sehemu nyingine na aliporudi akakuta jirani yake alishafungua kesi na hukumu ilishatolewa ya kuuza nyumba hiyo.