Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Matemanga wilayani Tunduru,wakilisukuma gari jipya la kubebea wagonjwa lililotolewa na serikali litakalotumika kuboresha huduma bora za matibabu katika kituo cha afya Matemanga.
Mganga mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Wilfred Rwechungura kulia,akipokea funguo la gari la kubebea wagonjwa (Ambulance)kutoka kwa Mbunge wa jimbo la Tunduru Kaskazini lililotolewa na serikali ili kurahisisha na kuboresha huduma za afya katika kituo cha afya Matemanga wilayani humo.
Picha no 176 Mfamasia wa kituo cha afya Matemanga wilayani Tunduru mkoani Ruvuma Aden Mundu kushoto,akimuonyesha Mbunge wa jimbo la Tunduru baadhi ya dawa zinazohifadhiwa katika chumba kidogo chenye mwanga hafifu kutokana na kukosekana kwa chumba maalum cha kuhifadhi dawa na hata kusababisha baadhi ya dawa kuharibika,katikati mganga mfawidhi wa kituo hicho Dkt Daniel Mwakipa.
………..
Na Mwandishi wetu, Tunduru
MBUNGE wa Jimbo la Tunduru Kaskazini Hassan Kungu,amekabidhi gari la kubebea wagonjwa kwa kituo cha afya Matemanga ili kurahisisha usafirishaji wa wagonjwa wanaopewa rufaa au wanaotakiwa kufuatwa majumbani ili kuwahishwa Hospitali kwa ajili ya kupata huduma za matibabu.
Akikabidhi msaada huo kwa mganga mkuu wa wilaya ya Tunduru Dkt Wilfred Rwechungura,Kungu alisema, kuwa gari hilo litasaidia kutatua changamoto ya muda mrefu ya wagonjwa kutoka tarafa ya Matemanga wanaotakiwa kwenda Hospitali ya wilaya Tunduru mjini umbali wa kilomita 65 au Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Ruvuma(Homso)iliyopo umbali wa kilomita 180 ili kupata huduma zaidi za matibabu.
Aidha alisema,gari hilo litamaliza changamoto kwa mama wajawazito kutumia usafiri wa pikipiki na bajaji wanapotaka kwenda Hospitali ya wilaya kwa ajili ya kujifungua na kusisitiza kuwa, ni muhimu gari hilo litunzwe ili liweze kusaidia mkakati wa serikali wa kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Kungu,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake kwa kutoa fedha zilizowezesha kupata gari hilo ambalo litasaidia sana kupunguza mateso na vifo kwa wananchi kufia njiani kwa kutofika kwa wakati katika vituo vya kutolea huduma za afya kutokana na kukosa usafiri wa uhakika.
Ameikumbusha ahadi ya Rais Dkt Samia Suluh Hassan aliyotoa wakati akiwa makamu wa Rais ya kujenga wodi maalum ya mama na mtoto katika kituo cha afya Matemanga ili wajawazito wapate sehemu nzuri na salama ya kujifungulia badala ya kutumia wodi mchanganyiko.
Katika hatua nyingine Kungu alisema,serikali imeanza upanuzi wa mradi wa maji Milonde ambao kwa sasa wataalam kutoka wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wanaendelea na kazi ili mradi huo ili uweze kutosheleza mahitaji ya wakazi wa kata hiyo na maeneo mengine ya jirani.
Amewataka wananchi,kuiunga mkono serikali ya awamu ya sita ambayo tangu ilipoingia madarakani miaka mwili iliyopita, imeonyesha upendo mkubwa kwa kutoa fedha zilizoboresha huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo afya,maji na elimu.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya ya Tunduru Dkt Wilfred Rwechungura alisema,kupatikana kwa gari hilo kunaifanya wilaya ya Tunduru kuwa na magari manne ya kubebea wagonjwa yaliyosambazwa katika vituo mbalimbali vya afya.
Rwechungura alisema, Halmashauri ya wilaya kupitia idara ya afya imepokea zaidi ya Sh.bilioni 2.6 ili kuimarisha na kuboresha huduma za afya ikiwemo kujenga zahanati 19 na vituo vya afya 5.
Kwa mujibu wa Dkt Rwechungura,kwa mwaka 2022/2023 walipokea Sh.milioni 400 zilizotumika kununua vifaa tiba na mwaka 2023/2024 tayari serikali imetenga jumla ya Sh.milioni 700 ili kununua vifaa tiba kwenye zahanati na vituo vya afya vyenye uhitaji.
Pia alisema,katika kipindi cha miaka miwili wamepokea jumla ya watumishi wapya 122 wa kada mbalimbali ambapo uwepo wa watumishi hao kumeleta tija kubwa kwa sekta ya afya katika wilaya ya Tunduru.
Dkta Rwechungura amewataka wananchi wa Tunduru kutumia zahanati,vituo vya afya na Hospitali za serikali zinazojengwa na kufanyiwa ukarabati kwenda kupata huduma bora ili kuondokana na changamoto za afya.
Diwani wa viti maalum tarafa ya Matemanga Sitawa Timamu alisema,gari hilo litaokoa maisha ya wanawake wajawazito wanaopoteza maisha wakiwa njiani wanapokwenda kwenye vituo vya afya na Hospitali kwa kutumia usafiri wa boda boda na baiskeli.
Timamu,ameishukuru serikali kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa majengo mapya katika kituo hicho cha afya,hata hivyo alieleza kuwa kituo hicho bado kinaelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa wanaokwenda kupata huduma.
Ameiomba serikali ,kuongeza majengo ikiwemo wodi za kulaza wagonjwa katika kituo hicho ambacho kinakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya kutolea huduma,kwani sasa kitanda kimoja kinatumika na wagonjwa zaidi ya watatu kwa wakati mmoja.
“tunaishukuru serikali imeleta mashine ya kufualia nguo katika kituo chetu cha afya Matemanga,hata hivyo mashine ile haijaanza kutumika kwa sababu ya kukosa sehemu ya kuiweka badala yake tangu ilipofika imewekwa chini na haitumiki”alisema Timam.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Yusuf Mabena,amempongeza Kungu kwa kutimiza ahadi zake kwa wananchi wa jimbo la Tunduru,na amewataka wanachama wa chama wa CCM na wananchi wa wilaya hiyo kumuamini na kumuunga mkono Mbunge wao.