Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na viongozi mbalimbali wakati alipowasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam kufungua Jukwaa la Kodi na Uwekezaji kwa Mwaka 2024. Tarehe 27 Februari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa wadau wa sekta ya fedha wakati akikagua mabanda ya maonesho katika Jukwaa la Kodi na Uwekezaji kwa Mwaka 2024 linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Tarehe 27 Februari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwaongoza viongozi na washiriki mbalimbali wa Jukwaa la Kodi na Uwekezaji mwaka 2024 katika kuimba wimbo wa Taifa wakati wa ufunguzi wa Jukwaa hilo uliyofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Tarehe 27 Februari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Ufunguzi wa katika Jukwaa la Kodi na Uwekezaji kwa Mwaka 2024 linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Tarehe 27 Februari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizindua Jukwaa la Kodi na Uwekezaji kwa Mwaka 2024 linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Viongozi wengine ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Zena Said, Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Waziri wa Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo. Tarehe 27 Februari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa wafanyabiashara mara baada ya kufungua Jukwaa la Kodi na Uwekezaji kwa Mwaka 2024 linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Tarehe 27 Februari 2024.
…………..
Na Sophia Kingimali
MAKAMU wa Rais Dk.Philip Mpango amesema Tanzania imeendelea kuwa kitovu cha uwekezaji na nchi yenye uchumi unaokuwa kwa kasi Kusini mwa Jangwa la Sahara, licha ya misuko suko ya uchumi na kijamii inaayoendelea duniani kote
Hayo ameyasema leo Februari na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango alipomwakilishwa Rais Samia Suluhu Hassan katika Jukwaa la Uwekezaji na Kodi 2024 lililofanyika Leo februari 27,2024 katika kituo cha mikutano cha kimataifa ya Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa Serikali imeendelea kufanya maboresho ya sera na kanuni ili kutatua changamoto za uwekezaji na wafanyabiashara ili waweze kulipa kodi kwa hiari na kuiwezesha Serikali kutekeleza mahitaji kwa Umma.
Aidha Dkt Mpango ameongeza kuwa, Jitihada hizo za Serikali ambayo imekuwa ikishirikiana na sekta binafsi imepaisha makusanyo ya mapato yaliyotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na hiyo ni pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei uliofikia asilimia 3.2 kwa mwezi Julai hadi Desemba 2023 kiwango ambacho kipo ndani ya lengo la kati ya asilimia 3 hadi 7.
“Makusanyo ya shilingi Trilioni 22.6 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 yalipelekea kuongezwa kwa Bajeti kuu ya Serikali kutoka shilingi Trilioni 36 mwaka 2021/2022 hadi Trilioni 44.4 mwaka 2023/2024 ambazo zimesaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo reli ya kisasa ya SGR ambayo imefanyiwa majaribio ya mafanikio jana, ukarabati wa miundombinu ya bahari na maziwa makuu, pamoja na asilimia 79 ya vijijini kufikiwa na huduma ya maji.” Amesema.
Aidha amesema kuwa, Serikali imeendelea kuboresha sekta ya afya kuanzia ngazi ya Taifa hadi vituo vya afya kwa kuzingatia upatikanaji wa vifaa tiba, dawa pamoja na rasilimali watu huku katika sekta ya Elimu Rais Samia akiongeza wigo wa elimu bure hadi sekondari, miundombinu ya kufundishia na kujifunza, kutatua changamoto ya uhaba wa walimu pamoja na kuongeza idadi ya wanufaika wa mikopo ya Elimu ya juu.
Kuhusiana na jukwaa hilo, Mpango amesema hiyo ni fursa kwa wadau kutoa maoni ya kodi na uwekezaji katika kuelekea bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2024/2025.
” Maoni haya yatatumika katika mchakato wa bajeti inayofuata… Bila uwekezaji hakuna kodi Mawaziri wa Fedha zingatieni maoni ya sekta binafsi na walipa kodi, Tuwe wanyenyekevu tuwasikilize walipa kodi na wawekezaji nakufanyia kazi mapendekezo yao ili tutengeneze vivutio vipya na kupata wawekezaji wapya nakutimiza lengo la kufikia kipato Cha kati mwaka 2025.” Amesema.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imekuwa ikiweka kipaumbele katika masuala ya uwekezaji na ufanyaji biashara kwa kuweka mazingira wezeshi na katika sera za Kodi Serikali imekuwa ikielekeza kukusanya kodi kwa weledi, kutoa elimu, kusimamia sera ya ulipaji kodi na Usajili wa walipa kodi mpya.
Amesema, ushirikishwaji huo utasaidia kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo kulipa kodi kwa hiari pamoja na kutoa risiti kwa kila bidhaa inayonunuliwa huku changamoto ya kimfumo au mashine kuharibika ikiwa moja ya sababu ya ukwepaji ulipaji kodi kwa hiari.
Akizungumzia ukadiliaji wa kodi Dkt Nchemba amesema TRA inakamilisha kujenga mfumo rasmi wa ukadiliaji huku ofisi ya msuluhishi wa masuala ya Kodi tayari imeanza kufanya kazi ya kutatua migogoro ya kikodi.
Naye,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais; Sera, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema kwa miaka mitano ( 2019/2023) maboresho na mabadiliko 665 ya Sera, Sheria na kanuni za kodi na yasiyo ya kikodi yamefanyika na yote yamelenga kuboresha mazingira na kuvutia wawekezaji.
Prof. Kitila amesema Tanzania ina mvuto na mazingira mazuri ya uwekezaji na kupitia jukwaa hilo watapokea maoni mengi zaidi kwa lengo la kuvutia uwekezaji na ufanyaji biashara kwa wingi zaidi ili kodi itakayokusanywa iweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF,) Raphael Maganga amesema; sekta binafsi nchini inatambua jitihada za Serikali katika kuboresha uchumi, kutambua mchango wa TPSF na kuitangaza nchi kimataifa kwa manufaa ya wananchi.
Amesema, Jukwaa hilo limelenga kuimarisha ushirikiano baina ya Sekta za Umma na binafsi katika kuboresha uchumi, kupokea maoni ya wadau na kujumuisha wadau katika maandalizi ya bajeti kuu ya Serikali, na kueleza kuwa sekta binafsi inatambua jitihada za Serikali katika ukusanyaji wa kodi na TPSF imekuwa ikichangia asilimia 90 ya Kodi inayokusanywa.
Aidha amesema, jukwaa hilo ni muhimu kwa wadau katika kuboresha uchumi wa nchi na kushauri Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA,) kukusanya Kodi kwa kutumia weledi, kutoa elimu kwa wafanyabiashara ambao jukumu lao ni kuendelea kulipa kodi pamoja na Serikali kutanua wigo wa sehemu za makusanyo ya Kodi.
Aidha Maganga, ameishauri Serikali kupitia mifumo na kuirahisisha sheria ya Kodi kwa wafanyabiashara wadogo pamoja na kuandika kwa lugha rahisi na TPSF itaendelea kutoa elimu ya ulipaji kodi kwa hiari na kuweka msimamo wa kutotambulika kwa wafanyabiashara wasiolipa kodi katika vyama vyao.
Awali Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu Mwamba alieleza kuwa jukwaa hilo limelenga kupata maoni ya wadau kuhusiana maboresho ya sera kodi kuelekea bajeti kuu ambayo pia itakasaidia kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
Jukwaa la Uwekezaji na Kodi kwa mwaka 2024 limebeba kauli mbiu ya ‘Maboresho ya Sera Katika Uwekezaji, Ukusanyaji Mapato ya Ndani na Ukuaji wa Uchumi Jumuishi.” Limeandaliwa na SJT na SMT kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo.