Na: Mwandishi Wetu, Tanga.
Mkoa wa Tanga umepata mafanikio makubwa dhidi ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU). Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini ambapo amesema katika mkoa wa Tanga, maambukizi yamepungua kutoka asilimia 4.4 hadi asilimia 2.9.
Waziri Ummy ametoa kauli hiyo Februari 23, 2024 wakati wa hafla ya kukabidhiwa vifaa vya kuboresha huduma za afya katika mapambano dhidi ya magonjwa ya VVU na kifua kikuu, hafla iliyofanyika katika Hospitali ya Rufani ya Bombo, jijini Tanga. Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) kupitia ufadhili wa Serikali ya Marekani kupitia kituo chake cha Kudhibiti na Kupambana na Magonjwa (CDC) limetoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo pikipiki 50, majokofu 72, sentimita 56, kompyuta 50, UPS 50 na printa 50 ambavyo vyote vimegharimu milioni 800.
Katika hafla hiyo, Waziri Ummy amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya Ukimwi ni endelevu na hivyo mkoa usibweteke kutokana na mafanikio hayo. “Hata kama maambukizi yamepungua katika mkoa wetu, tusibweteke, tunaomba kila mmoja wetu apime virusi vya Ukimwi ili kujua hali ya maambukizi na ukigundulika una maambukizi tunakuanzishia dawa ili uendelee kuishi maisha mazuri”, amesema Ummy.
Akipokea vifaa hivyo, Waziri Ummy amesisitiza kuwa watakaokabidhiwa vifaa hivyo wavitumie kama ilivyoelekezwa ili kuwafikia walengwa waliopo kwenye mazingira magumu na waishio mbali na vituo vya kutolea huduma za afya. Mafanikio dhidi ya VVU mkoani Tanga ni matokeo ya juhudi kubwa zinazofanywa na serikali kutoa elimu ya VVU kwa wananchi na uwekezaji mkubwa ulifanywa na serikali kupitia utoaji wa huduma bora kama vile upatikanaji wa uhakika wa dawa.