Arusha.Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa watu wasioridhishwa na maamuzi yanayotolewa katika mahakama kukata rufaa kwa kuwa ni haki yao.
Aidha Jaji Juma amewataka pia Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Majaji wote nchini kutoa haki kwa kuzingatia mizani ya haki bila kuyumbishwa na mitazamo inayotolewa na watu baada ya hukumu kusomwa.
Prof. Juma ameyasema hayo jijini Arusha wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania unaofanyika kwa siku tatu mkoani hapa.
Hata hivyo majaji hao wamekutana mkoani Arusha kwa lengo la kukumbushana na kubadilishana uzoefu kuhusu majukumu ya Majaji hao na nafasi zao katika maboresho ya Mahakama na kupitia maboresho ya Mhimili huo ili kufanikisha ustawi wa wananchi kwa ujumla.
Ameongeza kuwa ,Moja ya kazi za Majaji Wafawidhi ni kusimamia eneo la utoaji haki, na haki sio ushindi bali ni ushahidi unaotolewa kwa kuangalia mizani ya haki hivyo msikatishwe tamaa na wanaopinga maamuzi yanayotolewa.
“Nawaomba sana niwakumbushe kusimamia haki kwa kuhakikisha kuwa mnasoma taarifa mbalimbali zinazowasilishwa kwao ili kutatua changamoto zinazojitokeza na kuzitafutia ufumbuzi.”amesema.
“Mnatakiwa kusimamia utoaji haki sio kuwa sehemu ya malalamiko au kukaa na kusubiri taarifa za viongozi wanaowasaidia, mfano Wasajili, Watendaji na Mahakimu Wafawidhi, lazima unapopokea taarifa, ni muhimu utafute changamoto zilizojificha ambazo wewe kiongozi mkuu wa Kanda au Divisheni unatakiwa kuzifahamu na kuzitafutia ufumbuzi,” amesema Jaji Mkuu.
Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuwakumbusha Majaji Wafawidhi kuhusu matumizi ya TEHAMA hususani katika kipindi hiki ambacho Mahakama ipo kwenye safari ya kuelekea Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’.
“Matumizi ya Teknolojia ni eneo la msisitizo ambalo uwekezaji mkubwa umefanywa. Ni wajibu wetu Viongozi kuhakikisha kuwa, miundombinu yote ya TEHAMA na vifaa vilivyofungwa vinatumika kuleta manufaa makubwa na kutusaidia kuifikisha Mahakama katika hadhi ya Mahakama Mtandao,” ameeleza Mhe. Prof. Juma.
Ameongeza kwamba, matumizi ya Teknolojia ndio nyenzo ya karne ya 21 ya kuleta matokeo makubwa ya kusogeza huduma za haki zilizo bora, hivyo Taaluma ya Sheria na Mifumo ya utoaji haki haiwezi kukwepa mapinduzi makubwa yanayotokana na Teknolojia kukua kwa kasi.
Amewasihi Majaji hao kuwa sehemu ya safari ya Mahakama ya Tanzania inayolenga kutumia mifumo ya teknolojia kudijiti nyaraka zote za Mahakama ili kuleta mabadiliko makubwa katika utoaji huduma.
Ametaja faida kadhaa zitakazopatikana endapo Mahakama itadijiti nyaraka zake, ambazo ni pamoja na kuondoa changamoto za nyaraka kutoonekana kwa kuhakikisha kuwa nyaraka zote zinatunzwa katika mifumo ya kielektroniki, kuimarisha ufanisi katika hatua za kimahakama zinazopitiwa hadi haki kupatikana.
Faida nyingine ni kuimarisha upatikanaji wa taarifa muhimu za mashauri ya wadau, Majaji, Mahakimu, Wanasheria, Wadaawa na wananchi kwa ujumla, kuongeza uwazi kwa kuweka kumbukumbu kuhusu usajili wa mashauri, amri na maamuzi mbalimbali yanayotolewa, kuongeza uwajibikaji pamoja na kuiwezesha Mahakama kukusanya na kuchambua takwimu kuhusu mashauri.
Kadhalika amewataka, Majaji hao kuwatumia Maafisa TEHAMA kikamilifu ili kutoa suluhisho ya changamoto mbalimbali za Mifumo ya Kieletroniki inayotumika mahakamani ikiwemo Mfumo wa Kieletroniki ya Usimamizi wa Mashauri (e-CMS), Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) na mingine.
Akizungumzia kuhusu Mfumo wa ‘e-CMS’ Jaji Mkuu amewataka Majaji hao kuendelea kuutumia na kubaini changamoto zinazohusiana na Mfumo huo. Hata hivyo amesema amepata changamoto na mapendekezo kuhusu Mfumo huo kutoka kwa Jaji Mfawidhi Kanda ya Mwanza.
“Jaji Mfawidhi Kanda ya Mwanza, alipendekeza suluhisho katika changamoto za Mfumo wa ‘e-CMS’, ambapo amependekeza Wataalamu wa Mahakama wafuatilie kwa karibu na kwa haraka uwezekano wa kuongezewa uwezo wa kuhifadhi ‘data’,” ameeleza Jaji Mkuu.