Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mara baada ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na TASAF mkoani Iringa.
Sehemu ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao katika eneo la Migori mkoani iiringa.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mhe. Veronica Kessy akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (hawapo pichani) kabla ya kumkaribisha Waziri Simbachawene kuzungumza nao mkoani humo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa na baadhi ya wananchi akikagua mradi wa birika la kunyweshea mifugo lililojengwa na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kijiji cha Kinywang’anga kilichopo mkoani Iringa
Sehemu ya birika la kunyweshea mifugo lililojengwa na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kijiji cha Kinywang’anga kilichopo mkoani Iringa.
………………..
Na.Lusungu Helela
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameutaka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuweka nguvu zaidi katika kuziingiza kaya maskini zenye watu wenye ulemavu kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini ili nao waweze kujiinua kiuchumi na kufikia malengo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anatamani kuona mpango huo unagusa makundi mengi zaidi yenye uhitaji.
Mhe. Simbachawene ameyasema hayo leo alipotembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Kijiji cha Kinywang’anga Wilaya ya Iringa, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani humo ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na TASAF.
Amesema TASAF imekuwa mkombozi kwa wananchi wanaonufaika kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na mpango huo huku akisisitiza kuwa katika awamu ijayo iwaangalie zaidi watu wenye ulemavu kwani wamekuwa wakikosa fursa nyingi kulingana na changamoto walizokuwa nazo.
“Kaya zenye watu wenye ulemavu na hazijiwezi kimaisha zina mzigo mara mbili ukilinganisha na kaya zisizojiweza na hazina watu wenye ulemavu, hivyo ni lazima kaya zenye walemavu zipewe kipaumbele zaidi” amesisitiza Mhe.Simbachawene
Amesema moja ya dhamira Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kaya maskini zenye walemavu zinapata uhakika wa milo mitatu kama zilivyo kaya nyingine masikini.
Hata hivyo Mhe.Simbachawene amesema Serikali inafanya kazi kubwa ya kuhakikisha fedha zinazotoka zinafika kila mahali na kwa walengwa sahihi hasa waishio vijijini katika kuboresha maisha ya Watanzania kupitia miradi mbalimbali ikiwemo ya TASAF.
Amesema miradi inayotekelezwa na TASAF inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja na kushirikisha jamii katika uhalisia wake akisema huo ndio msingi wa viongozi wa Tanzania.
“Lengo la miradi la TASAF ni kuondoa umasikini wa kipato kwa mtu mmoja mmoja na kaya, ndio maana kuna wanufaika wanaopewa fedha za moja kwa moja ili kuwapa ahueni katika hali zao za maisha,” amesema Mhe. Simbachawene.
Katika ziara hiyo, Mhe. Simbachawene alitembelea mradi wa ujenzi wa birika la kunyweshea mifugo katika Kijiji cha Kinywanga’nga akiguswa na utekelezaji wa mradi huo ambao unakwenda kuinua sekta ya uvuvi na kugusa moja kwa moja maisha ya wafugaji.
Awali Meneja wa Miradi ya Ajira za Muda Mfupi kutoka TASAF, Bw. Paul Kijazi amesema Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ina afua tatu katika jamii ikiwemo ya kuhawilisha fedha inayotolewa kwa wananchi wa kaya zisizokuwa na uwezo wa kufanya kazi wakiwemo wazee.
“Katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa tuna vijiji 134 vyote vinahawilishiwa fedha, tumeshaleta shilingi bilioni 3.663 katika awamu ya pili ya TASAF kwa walengwa, lakini pia tulileta fedha shilingi bilioni 1.09 kwa ajili ya vifaa vilivyotumika katika ajira za muda mfupi.