Na Ashrack Miraji Kilimanjaro
Mwandishi wa Fullshangwe alitembelea kwenye kijiji cha Singa wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro na kupita katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye maeneo ya biashara na baadhi ya familia na kushuhudia bomba za maji zikiwa hazitoi maji.
Hata hivyo, alizungumza na baadhi ya wananchi wa kijiji hicho ambapo wameeleza kuwa, licha ya kuchangia Sh162,000 kwa ajili ya kuunganishwa na huduma ya maji mwaka 2018 hawajawahi kupata huduma hiyo na kwamba wanalazimika kunywa maji ya mto Karanga hali ambayo inatishia usalama wa afya zao.
Mwananchi huyo ambaye ni mdau wa maendeleo hapa nchini, Joseph Mushi amefikia atua ya kuwasaidia wananchi hao kulipa gharama za Maji kwa Mwaka mzima amechukua hatua hiyo baada ya kuona wananchi wa kijiji hicho wanataabika kwa muda mrefu bila kuwa na huduma ya maji hali ambayo huwalazimu kunywa maji yasiyo safi na salama kutoka mto Karanga.
Akizungumzia kukerwa na changamoto hiyo ya maji mdau huyo joseph Mushi amesema kila mara wanapokuja likizo kijijini hapo kunakuwa hakuna maji hali ambayo imekuwa ikiwapa changamoto na wakati mwingine kushindwa kufanya shughuli za maendeleo.
“Kijiji hiki cha Singa ni kijiji ambacho kilikuwa na maendeleo makubwa sana kipindi cha nyuma ukilinganisha na maeneo mengine yote hapa Kilimanjaro, wakati baba zetu, babu zetu na babu wa babu zetu wanaongoza haya maeneo kulikuwa hakuna changamoto ya maji, sasa baada ya kijiji hiki kuingiliwa na watu wenye tamaa ndio tumefika hapa tulipofika,”
“Mama zetu na ndugu zetu wanateseka na hii hali, na sehemu yoyote ambayo hakuna maji, hakuna maendeleo yoyote yanayoweza kuja na sisi wananchi ambao tupo nje ya kijiji hiki hatutakubali ndugu zetu wataabike, hakuna sababu ya kukosa maji hapa kijijini kwasababu maji yetu hayatumii umeme, kwa sababu yanatoka milimani,”
Amesema kwa taarifa alizonazo katika kijiji hicho ni kwamba wananchi zaidi ya 400 wamefungiwa huduma ya maji kwa Sh162,000 na kwenye mabomba yao hakuna maji, yakitoka maji kwa mwezi ni mara moja au yasitoke kabisa na kwamba jambo hili sio sawa hata kidogo kwa kuwa wananchi mwanzoni walikuwa na mradi wao wa maji na walikuwa hawana changamoto ni baada ya mradi huo kusimamiwa na taasisi inayoitwa sikika.
“Wazazi wetu walitusomesha ili tuje tuwasaidie, sasa hii habari ya maji itaenda kuisha, lakini wakati tukipambana kuona ni namna gani ya kurejesha mradi wetu wa maji wa kijiji katika mstari, nitawalipia wananchi maji kwa mwaka mzima, na hawa wanaosimamia mradi wa maji kijijini kwetu wajitoe hawana msaada, ila tutapambana nao turejeshe hali yetu kama ilivyokuwa hapo zamani,”
Mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, Mathew Shio, amesema suala la maji kijijini hapo limekuwa likiwaumiza kichwa na kwamba shuguli za maendeleo zinashindwa kufanyika kutokana n kukosekana kwa huduma ya maji.
“Namuunga mkono asilimia 100, maana kwa ujanja ujanja ambao upo hapa kijijini kuhusu miradi wa maji hatutoboi, Kama huyu ndugu yetu ataweza kutuhudumia mwaka mzima tutatoboa, maana kero ya maji ni kubwa, ukienda kwenye shughuli za biashara maji hakuna, wafu wanatumia maji ya mto Karanga kunywa na kupikia, hii ni hatari sana kwa afya zetu.”
Mwenyekiti wa kitongoji Singa Kifueni, Joseph Ngowi amesema mradi wa maji uliopo kijijini hapo ambao unasimamiwa na taasisi ya Sikika haina maana kuwepo katika kijiji hicho kama wananchi wanaendelea kutaabika kiasi hicho.
“Waturudishie mradi wetu wa maji maana sisi wanakijiji hatuoni manufaa ya hawa wanaosimamia mradi huu, hatuwezi kuendelea kuteseka kwa sababu ya watu wazembe na wanaotuhujumu,”