Akizungumza Februari 25, 2024 na waumini wa Kanisa hilo wakati wa ibada ya Jumapili, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP THEOPISTA MALLYA amesema waumini wanapaswa kuwa na fikra na mitazamo chanya yenye kujenga jamii.
“Kitendo cha baadhi ya waumini kutofikiri kwa makini na kuwashirikisha watu wengine pindi wapatapo changamoto mbalimbali katika maisha hupelekea kufanya maamuzi mabaya yenye kuleta madhara katika jamii kama kujiua, kuiba, kudhulumu mali za wajane na yatima, na kufanya watoto wa mtaani kuongezeka katika jamii kitendo kinachopelekea watoto hao kufanyiwa ukatili wakiwa mitaani” alisema Kamanda Mallya
Sambamba na hayo Kamanda Mallya amewataka waumini kuwashirikisha viongozi wa dini pindi wanapopata changamoto mbalimbali ili wapatiwe ushauri wa kiroho ambao ni muhimu kwa kila muumini anapopitia nyakati hizo.
Nae Mchungaji wa Kanisa hilo NSUBHILEN NDENGAWA aliwataka waumini hao kujitokeza kwenye maeneo yao pindi waonapo au wafanyiwapo vitendo vya kihalifu na kikatili ambapo aliwasisitiza wakemee bila woga kwani kwa kufanya hivyo kutapunguza uhalifu na kuiacha jamii ikiwa salama.
Aidha alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kuendelea kuyafikia makundi mbalimbali kwa kutoa elimu ili jamii iachane na ukatili pamoja na matendo ya kihalifu ambayo hayampendezi Mungu na kuzingatia mafundisho yaliyoandikwa katika Kitabu kitakatifu (Biblia) hasa makatazo kama Walawi 18:22, Warumi 1:24-29, Zaburi 15:5, Kutoka 23:8, Kumbukumbu la Torati 16:19 na Waefeso 4:26.
Pamoja na kushiriki katika ibada, SACP. Mallya hutumia nyumba za ibada kama sehemu ya kutoa elimu ambayo waumini huwajengea imani ya kiroho ili kutoshiriki na kuchukia aina yeyote ya uhalifu katika jamii.