Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM jimbo la Kavuu wakati wa mkutano mkuu wa CCM jimbo hilo, Februari 25, 2024 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya Wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM jimbo la Kavuu wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa Kassim Majaliwa alipozungumza nao leo Februari 25, 2024 mkoani Katavi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM jimbo la Kavuu wakati wa mkutano mkuu wa CCM jimbo hilo, Februari 25, 2024 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………..
WAZIRI MKUU na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kinara katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
“Ni ukweli usiopingika kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama chetu amekuwa kielelezo cha mafanikio makubwa yanayofikiwa na nchi yetu kwa sasa.”
Amesema tangu Dkt. Samia ashike madaraka ya Urais, ameendelea kutekeleza miradi yote ya kimkakati kama Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 ilivyoelekeza.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo, (Jumapili 25, Februari 2024) katika Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Kavuu, uliofanyika kwenye shule ya sekondari ya Mizengo Pinda iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, katika Wilaya ya Mlele, mkoani Katavi.
“Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ikiwemo upatikanaji wa huduma za afya, kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa, Kanda na rufaa.”
Amesema pamoja na mafanikio mengine, Rais Samia ameimarisha diplomasia ya kiuchumi na nchi mbalimbali sambamba na kukuza utalii, lugha ya Kiswahili na masoko ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kukiamini Chama cha Mapinduzi kwani wakati wote kimeendelea kuwa nguzo ya kuwaunganisha Watanzania katika kujenga Taifa linalojitegemea kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni, na Taifa lenye umoja, amani, utulivu na mshikamano.
“Taifa hili, chini ya Serikali za CCM tuna uwezo mkubwa wa kujitegemea na kujiletea maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii. Haya yamedhihirika kupitia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika ujenzi wa Taifa letu na kuboresha maisha ya Watanzania katika nyanja mbalimbali.”
Amesema Chama cha Mapinduzi kimekuwa nguzo ya amani, umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania na hivyo kuwa chachu ya maendeleo nchini. “Umuhimu wa chama chetu, umeendelea kuonekana kwa jinsi ambavyo kimekuwa kikiwatumikia Watanzania huku nchi yetu ikidumisha umoja na amani miongoni mwa wananchi.”
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geoffrey Pinda alisema Jimbo la Kavuu na Halmashauri ya Mpimbwe kwa ujumla wamepiga hatua kubwa katika utekekezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwenye sekta za afya, elimu, miundombinu na maendeleo ya jamii.
Amesema, zaidi ya shilingi bilioni 1.2 zimetolewa kugharamia elimu bila malipo na shilingi milioni 238 zimetumika kukarabati shule kongwe.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, alisema shilingi bilioni 800 zimepokelewa kwa kwa ajili ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM na kuahidi kuwa wataendelea kusimamia Ilani hiyo pamoja na fedha zinazoletwa na Serikali kutekeleza miradi mbalimbali.
Awali, akiwa njiani kuelekea Mpimbwe, Mheshimiwa Majaliwa alisimama na kuzungumza na wananchi wa eneo la Sitalike ambapo pamoja na mambo mengine, amewasihi wawe wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kutatua mgogoro wa ardhi katika eneo hilo.