Na. Mwandishi wetu – Same.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ametoa rai kwa Wananchi wote nchini, Taasisi za Umma na Binafsi na Wizara mbalimbali nchini kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kutembelea vivutio vya utalii vinavyopatikana Tanzania.
Wito huo ameutoa jana Februari 23, 2024 wakati wa Uzinduzi wa Tamasha la Utalii lilojulikana kama ‘Same Utalii Festival’ lililobebwa na kaulimbiu isemayo “Alianzisha mama, Sisi Tunaendeleza” linalofanyika kwa siku 2 wilayani Same mkoani Kilimanjaro.
Imeelezwa kuwa kupitia tamasha hilo zaidi ya watalii wa ndani 180 wametembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii vilivyopo wilayani humo ambapo 88 kati ya hao wametembelea Hifadhi ya Taifa Mkomazi.
“Ni lazima tuvipende na kuvithamini vya kwetu kabla ya mtu wa nje kuvitangaza na kuvitembelea sisi wenyewe tuoneshe mfano. Usipokithamini ulichonacho nani atakithamini, naomba nitoe rai kwenu nendeni mkavitangaze vivutio hivi tulivyo barikiwa na Mungu ambaye alitupa tunu za Taifa letu,” alisema Mh. Kairuki.
Aidha, Waziri Kairuki amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele kuvitangaza vivutio vya utalii na kuhakikisha sekta ya utalii inaendelea kukua na kuendelea kuchangia katika pato la Taifa.
Awali akizungumza kumkaribisha mhe. Waziri, Kamishina wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Tanzania (TANAPA) Mussa Nassoro Kuji aliwapongeza watanzania wote waliojitokeza kwenda kutembelea Hifadhi ya Taifa Mkomazi kupitia tamasha hilo huku akisema, TANAPA itaendelea kuboresha miundombinu katika hifadhi zote ili kurahisisha shughuli za Utalii na Uhifadhi.
“Tunataka mtalii pindi aingiapo hifadhini afurahie kila sekunde na kila hatua hivyo utaona katika hifadhi hii na utaona kwa kipindi hiki kifupi tumetekeleza miradi ya bilioni 4 ambayo inahusisha ujenzi wa malango, viwanja vya ndege, ukarabati wa barabara, uzio wa kwa ajili ya faru, maji, nyumba za watumishi na tufanya haya katika Hifadhi zote za Taifa” alisema Kamishina Kuji.
“Tumejenga uzio wa kilometa za mraba 54 mahususi kwa ajili ya kulinda faru weusi na kutekeleza mradi maalum wa faru hao ambao tuliuanzisha mwaka 202, mradi huu uliochochea kwa kiasi kikubwa kuvutia watalii wengi hivyo basi, kama Shirika tutaendelea kulinda tunu hizi za Taifa kwa manufaa ya vizazi na vizazi” aliongeza Kamishina Kuji.
Wilaya ya Same iliyopo Mkoani Kilimanjaro ni miongoni mwa Wilaya yenye vivutio vingi ikiwemo Hifadhi ya Taifa Mkomazi inasifika kwa kuwa na Faru weusi wengi wanaoonekana kwa urahisi zaidi.