Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Kongwa-Dodoma.
Afya ni mtaji namba moja katika maisha ya mwanadamu. Afya bora ni msingi wa maendeleo kwani binadamu anapokuwa na afya bora inamwezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na hivyo kuchangia katika ujenzi wa maendeleo ya Taifa lake. Ndiyo maana wataalamu wa afya wanashauri wananchi kuwa na utamaduni wa kupima afya zao hata kama hawaumwi ili kuwa na uhakika wa afya njema na pale wanapobainika kuwa ni wagonjwa wa ugonjwa fulani, basi wanakuwa katika nafasi nzuri ya kuudhibiti kwani wataanza matibabu mapema.
Kutokana na unyeti wa afya, serikali kwa kushirikiana sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo wanashirikiana katika uboreshaji wa sekta ya afya ili kuhakikisha afya za wananchi zinakuwa salama ili pindi wananchi watakapohitaji huduma za afya, waweze kuzipata mahali popote walipo. Utoaji wa huduma za afya kwa wananchi unakwenda sambamba na uwepo wa vipaumbele ili huduma zitolewazo ziweze kuwa na tija katika maisha ya wananchi.
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imebainisha vipaumbele sita vya kisera katika sekta ya afya kwa mwaka 2024/2025. Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Kisera wa 23 wa Sekta ya Afya uliofanyika Jijini Dodoma Februari 15, 2024, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni: Raslimali watu, ubora wa huduma za afya, utekelezaji wa sheria ya Bima ya Afya kwa wote, wahudumu wa Afya ngazi ya jamii, mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi katika utoaji huduma za afya.
RASLIMALI WATU.
Raslimali watu ni nyenzo muhimu katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi. Na ili wataalamu wa afya waweze kutoa huduma bora ni muhimu kujengewa uwezo kwa kupata mafunzo ya muda mrefu na mfupi ili kuendana na mahitaji na mazingira ya utoaji huduma bora za afya. Katika Mkutano huo, Waziri Ummy alisisitiza kuwa kipaumbele cha kwanza ni raslimali watu katika afya. “Serikali imejitolea kuwekeza katika mafunzo na maendeleo ya watumishi wa Afya ili kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wananchi” amesema Ummy. Hivyo basi, kitendo cha serikali kutoa kipaumbele katika kuwajengea uwezo raslimaliwatu kwa maana ya wataalamu wa afya, ni mwelekeo mzuri wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
UBORA WA HUDUMA ZA AFYA.
Serikali inafanya juhudi kubwa za kuboresha ubora wa huduma za afya ili wananchi waweze kufurahia huduma hizo pindi wanapokwenda kupata huduma katika vituo vya kutolea huduma. Ubora wa huduma unakwenda sambamba na wagonjwa kupokewa, kusikilizwa na kuhudumiwa vizuri, kupata huduma stahiki ikiwemo kupata dawa zote muhimu ndani ya kituo cha kutolea huduma au hospitali na pia wagonjwa kuhudumiwa kwa wakati. Serikali pia inawajibika kununua vifaa tiba muhimu ili wagonjwa waweze kuhudumiwa kikamilifu. Katika Mkutano huo, Waziri Ummy alisema “Suala la ubora wa huduma za Afya tunaendelea kulisisitiza kwa kuzingatia umuhimu wa kuboresha huduma kwa wateja pamoja na kuhakikisha usalama wao ili mteja apate huduma iliyokuwa nzuri.”
UTEKELEZAJI WA SHERIA YA BIMA YA AFYA KWA WOTE.
Sera ya Bima ya afya kwa wote imelenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya pasipo kikwazo cha kiuchumi ili kuwa na afya njema ambayo ni msingi wa maendeleo. Kutokana na uwepo wa gharama katika kupata matibabu, bima ya afya ndiyo muarobaini wa kupata matibabu kwani bima itamwezesha mwananchi kupata matibabu ya uhakika muda wowote. Novemba 2, 2023 Bunge lilipitisha muswada wa Bima ya Afya kwa wote kwa asilimia 100 na Rais Samia Suluhu Hassan kutia saini na kuwa sheria kamili. Kwahiyo, utekelezaji wa sheria ya Bima ya Afya kwa wote kunatoa fursa ya upatikanaji wa huduma za afya za uhakika kwa Watanzania wote.
WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII.
Januari 31, 2024, kwenye Uzinduzi wa wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii uliofanyika katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar Es Salaam, Makamu wa Rais Dk. Philip Isdori Mpango alisema katika kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi kuanzia katika ngazi za chini kabisa, serikali imeamua kutenga bilioni 899.4 kwa ajili ya kuwajengea uwezo jumla ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wapatao 137,294 katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara. “Wahudumu wa Afya mtakaopewa dhamana ya kutekeleza jukumu hili zingatieni weledi na kujituma pamoja na kutoa rai kwa jamii kuupokea mpango huo na kuthamini huduma za wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii kwa kuwapa ushirikiano wa kutosha ili kulinda na kuboresha Afya katika jamii.” Amesema Makamu wa Rais Dk. Mpango. Uwepo wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ni hatua kubwa ya uboreshaji wa sekta ya afya kwa kuwafikia na kuwahudumia wananchi moja kwa moja kule walipo.
MAPAMBANO DHIDI YA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA.
Ongezeko la wananchi kuugua magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la juu ya damu (presha), saratani, magonjwa ya moyo, uzito uliopindukia, na kisukari kumeifanya serikali kuweka msukumo mkubwa katika kupambana na magonjwa haya kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuepuka magonjwa haya ambayo mtindo mbaya wa maisha, matumizi ya sigara, pombe, sukari na chumvi vimekuwa sababu kubwa. Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Prof. Mohamed Janabi ameshauri wananchi kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza kwa kufanya haya: Kutembea hatua 10,000 kwa siku, kula kwa wastani, kupunguza kula vyakula vya wanga, kuepuka vitu vyenye sukari, kupata muda wa kupumzika, kuepuka sigara, pombe na vyakula vya kusindika. Hivyo basi, Wizara ya Afya inatoa kipaumbele cha utoaji wa elimu na matibabu ili kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ambayo ni hatari kwa mustakabali wa afya za wananchi.
KUIMARISHA USHIRIKIANO KATI YA SERIKALI NA SEKTA BINAFSI KATIKA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA.
Katika kuhakikisha huduma bora za afya zinawafikia wananchi, serikali inaimarisha ushrikiano kati yake na sekta binafsi (Public and Private Partinership-PPP) ili kuweza kuendana na ongezeko la watu na mahitaji ya huduma za afya kwa wananchi. Watu binafsi, taasisi na asasi zisizo na serikali zinazo fursa ya kuwekeza katika sekta ya afya kwa kujenga hospitali, maabara, viwanda vya dawa na maduka ya dawa ili kusogeza huduma kwa wananchi. Hivyo basi, sekta ya afya ni miongoni mwa maeneo ambayo kuna fursa nyingi za uwekezaji. Februari 18, 2024, katika tukio la uzinduzi wa hospitali ya Saifee Tanzania ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inathamini na kutambua mchango wa sekta binafsi katika kuimarisha ustawi wa jamii na Watanzania. “Ni matumaini yangu kuwa Taasisi ya Saifee itasaidia kupunguza rufaa a wagonjwa kwenda nje ya nchi na kupunguza gharama kwa wananchi na serikali kwa ujumla, hivyo uwekezaji huu una manufaa makubwa sana kwa Taifa.” Kwa sasa asilimia 40 ya vituo vya afya hapa nchini, vinamilikiwa na sekta binafsi huku serikali ikimiliki vituo kwa asilimia 60.
Nihitimishe makala haya kwa kumpongeza Waziri wa Afya Ummy Mwalimu na timu yake nzima wizarani pamoja na wadau wengine kutoka sekta binafsi kwa ushirikiano wa pamoja uliowezesha wizara kuja na vipaumbele hivi sita ambayo kwa hakika vitasaidia katika kujenga afya bora za wananchi na hatimaye kufikia maendeleo ya nchi.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.