Na Issa Mwadanga-Songwe.
Wanawake Mkoani Songwe wametakiwa kuwashirikisha wenza wao wakati wanapochukua mikopo ya Ujasiriamali ili kuepusha matokeo hasi yanayotokea kwa baadhi yao wanaposhindwa kulipa mikopo hiyo.
Hayo yalisemwa tarehe 24 Februari 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP THEOPISTA MALLYA alipohudhuria Kongamano la Nishati Mbadala lililofanyika Vwawa Wilayani Mbozi lililoandaliwa na Taasisi isiyo ya kiserikali TANZANIA WOMEN EMPOWERMENT NETWORK (TAWEN) ambayo imeingia mkataba na kampuni ya usambazaji Gesi ORXY kwa lengo la kuunga juhudi za serikali kumtua mwanamke kuni kichwani.
Kamanda Mallya alisema “Kuna baadhi ya wanawake huchukua mikopo hatarishi bila kumjulisha mwenza wake ambayo mnashindwa kumudu malipo yake kitendo hicho kinapelekea kuwa na msongo wa mawazo na baadhi yao uanza kuua watoto wao kwa kuhisi watapata shida kisha anajiua na yeye, hiyo ni mbaya wanawake wenzangu mnatakiwa kuchukua mikopo yenye tija ambayo mnaweza kumudu kuilipa ikiwa ni pamoja na kumshirikisha mwenza wako” alisema Kamanda Mallya.
Sambamba na hayo Amewaasa wanawake wa mkoa huo kutumia nishati mbadala ili kuepuka athari zitokanazo na matumizi ya nishati ya kuni.
Nae Mratibu wa Kongamano hilo kutoka TAWEN Dar Es Salaam Levina Mlokozi akizungumza katika kongamano hilo ambaye ni mwakilishi wa Mkurugezi wa TAWEN alisema kuwa lengo la kongamano hilo ni kuhakikisha mama anatuliwa kuni kichwani ili kusababisha mazingira yanatunzwa na kuwa salama.
“Tumeandaa kongamano hili kuunga juhudi za Mh. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuwafanya wanawake wa Mkoa wa Songwe watumie nishati safi ambayo ni salama kwa afya yao” alisema Mratibu Mlokozi
Kongamano hilo lililobeba kauli mbiu isemayo “Kumtua mama Kuni Kichwani” ambapo jumla ya mitungi ya gesi 100 ilitolewa kwa wanawake Mkoani hapa kwa lengo la kuendelea kuiweka Tanzania ya kijani.