Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akizungumza na Wakuu wa Wilaya katika Kikao cha Kamati ya Wakuu wa Wilaya Zanzibar kilichofanyika Hoteli ya Diamonds Mapenzi Beach iliyopo Pwani mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja leo tarehe 24/02/2024.
……………………
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,amewasihi Wakuu wa Wilaya nchini kuongeza ubunifu na uchapakazi katika kusimamia na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Nasaha hizo amezitoa wakati akizungumza katika kikao cha Kamati ya Wakuu wa Wilaya Zanzibar kilichofanyika katika Hoteli ya Diamonds Mapenzi Beach iliyopo Pwani mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alieleza kuwa maendeleo yanayopatikana katika wilaya mbalimbali nchini yanatokana na kazi kubwa inayofanywa na Viongozi hao katika kufanikisha masuala mbalimbali ya kimaendeleo katika nyanja za kijamii na kisiasa.
Dkt.Dimwa,alisema Wakuu wa Wilaya wana wajibu wa kusimamia,kuratibu na kufanikisha kazi zote za Chama ndani ya maeneo yao ya kiutendaji na kwamba wamepewa jukumu Hilo kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 inayowatambua kuwa Wajumbe wa Kamati za Siasa za Wilaya Kichama.
Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo Dkt.Dimwa,alisema CCM ni ngazi baina ya Serikali na Wananchi katika kufanikisha utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kupitia Uchaguzi Mkuu uliopita kutia Ilani ya CCM.
Pamoja na hayo alisisitiza usimamizi wa ulinzi,usalama na maadili katika Wilaya mbalimbali ili kudhibiti vitendo vya uhalifu na ukiukaji wa mila na desturi za kijamii.
Aidha,aliwataka Wakuu wa Wilaya kusimamia na kutathmini mienendo, utendaji na tabia za watendaji wao katika sehemu za kazi ili kuimarisha nidhamu na uwajibikaji.
“Nakupongeze sana kwa kazi kubwa mnazofanya katika Wilaya zenu na ushauri wangu shukeni hadi ngazi za shehia kujua changamoto za wananchi na mzitafutie ufumbuzi iwe Serikalini au katika Chama.”,alisisitiza Dkt.Dimwa.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Wilaya Zanzibar ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “B” Hamida Mussa Khamis,amesema wamepokea maelekezo na ushauri uliotolewa na Naibu Katibu Mkuu Dkt.Dimwa na watayafanyia kazi ili yawe chachu ya kuongeza ufanisi katika utendaji wao wa kila siku.
Alisema kupitia kikao hicho kitafungua ushirikiano mpya wa kiutendaji baina ya watendaji,viongozi na wanachama wa CCM kuendelea kushirikiana vizuri na Wakuu wa Wilaya katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kikao hicho cha kutathmini masuala mbalimbali ya kiutendaji katika Wilaya za Zanzibar kinafanyika kila baada ya miezi mitatu kikishirikisha Wakuu wa Wilaya za Zanzibar zikiwemo Mjini,Magharibi ‘A’,Magharib ‘B’,Kati,Kusini Unguja,Mkoani,Wete,Micheweni,K askazini ‘A’,Kaskani ‘B’ na Micheweni.