Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC),Edwin Soko akizungumza katika mkutano wa wana habari ulioandaliwa na Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza ambaye ni Katibu Tawala (Miundombinu), Mhandisi Chagu Ng’oma,leo akimkaribisha Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla kuzungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi yake.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Amos Makalla, leo akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali mkoani humo.
Aliyekuwa Mkurugenza wa UTPC na Mwenyekiti mstaafu wa MPC, Abubakar Karsan,leo akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari uliondaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
………..
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
MKUU wa Mkoa wa Mwanza,Amos Makalla,amewaagiza viongozi wa serikali na wakuu wa taasisi zake akiemo wakurugenzi wa halmashauri za jiji,manispaa na wilaya,wasikalie taarifa wanazozihitaji waandishi wa habari,wazitoe kwa wakati kuepuka upotoshaji.
Pia kutokana na umuhimu mkubwa wa vyombo vya habari katika jamii na serikali,amewaahidi ushirikiano,kuhakikisha wanatumia kalamu zao kwa weledi wakizingatia miiko ya taaluma yao na hivyo kuiwezesha nchi kuwa salama na kupata maendeleo ya kijamii,kiuchumi na kisiasa.
Makalla ametoa maelekezo hayo leo katika mkutano na wanachama wa Chama Cha Waandishi wa Habari mkoani humu (MPC) wa vyombo mbalimbali,uliofanyika katika ukumbi mkubwa wa mikutano wa ofisi yake.
“Kukosa ushirikiano katika taasisi za serikali,nawaelekeza viongozi wote watoe taarifa kwa waandishi wa habari wanazozihitaji,wasizikalie,wazitoe wazipate kwa wakati bila kujali ni habari mbaya au nzuri,”amesema Makalla.
Amesema atatoa ushirikiano wa kutosha na katika kukabiliana na changamoto ya utandawazi,serikali itatoa taarifa haraka kuepuka upotoshaji unaofanywa hasa na mitandao ya kijamii na kutahadharisha,wasipozitoa waandishi wata provoke na kuzitoa.
“Natakiwa kumuunganisha Rais Dk.Samia Suluhu Hassan na wananchi kupitia waandishi wa habari walio daraja kati ya serikali na jamii kwa kutangaza mazuri yaliyofanywa na serikali.Upo umuhimu na mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika maendeleo ya nchi,”amesema Makalla na kusistiza ukosoaji chanya unakubalika na hilo litafanyiwa kazi.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema takwimu zinaonyesha Mwanza ni ya pili kwa wingi wa watu na kuchangia pato la taifa,hivyo mkakati na agenda yake ni kuufanya wa kwanza katika kuchangia pato hilo pia,kitovu cha Kanda ya Ziwa na Ukanda wa Maziwa Makuu.
“Mwanza imependelewa kwa miradi ya kimkakati ya ujenzi wa Daraja la JP Magufuli,SGR,Meli ya MV Mwanza,uboreshaji wa bandari na sasa ujenzi jengo la abiria lenye hadhi ya kimataifa.Rais amejitahidi sana na ameonesha dhamira ya kuufanya uwanja wa Ndege wa Mwanza kuwa wa kimataifa,”ameeleza
Makalla ameeleza zaidi kuwa mwelekeo wa pili ni mkakati wa kukuza utalii mkoani humu na tayari ameunda kikosi kazi cha kuandaa mkakati huo,ukikamilika utawashawishi watalii kuwa akishuka uwanja wa Ndege Mwanza baada ya saa moja atakuwa amewaona wanyama katika hifadhi ya Serengeti na vituo vingine.
“Tunataka kukuza utalii lakini kuna mambo mengi yanatakiwa.Rai yangu wawekezaji waje kuwekeza katika ujenzi wa kumbi kubwa za mikutano za kimataifa na hoteli za kitalii zenye hadhi ya kimataifa,”amesema na kuwataka waandishi wa habari kutangaza vivutio vya Mwanza na kuifanya kitovu cha Kanda ya Ziwa.
Akizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa Makalla amewaasa waandishi wa habari kutanguliza uzalendo na maslahi ya nchi na kuifanya Tanzania kubaki salama baada ya uchaguzi huo kumalizika.
Amedai kalamu za waandishi wa habari zinaweza kuufanya uchaguzi huo ukawa salama na nchi ikabaki salama,hivyo kila mtu aangalie Tanzania kwanza na kutahadharisha kuwa nchi zilizoharibikiwa chanzo ni kalamu.
“Niwashukuru kuona mko tayari kwa uchaguzi,hivyo tutangulize uzalendo,uchaguzi utapita nchi na Tanzania ibaki salama.Tutawapa ushirikiano na usalama wenu tutaendelea kuusimamia,”ameahidi Makalla.
Awali Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC),Edwin Soko amesema kupata taarifa katika taasisi za umma bado ni changamoto,wamegeuza utoaji taarifa ni hisani badala ya haki kwa mujibu wa Sheria ya Huduma ya Habari ya Mwaka 2016.
“Waandishi wa habari ni mdomo wa wasio na sauti na daraja kati ya wananchi na serikali.Kazi zimeleta mabadiliko na matokeo chanya yaliyoleta maendeleo.Bado sheria baadhi zinawakwamisha kutekeleza majukumu yao na tunamshuruku Rais Dk.Samia ameridhia kufanyika maboresho kwa baadhi ya sheria kikwazo,”amesema.
Kwa mujibu wa Soko, malengo ya MPC ni kufanya uandishi wa kuleta majawabu katika jamii badala ya kukosoa pekee,katika malengo ya maendeleo watazingatia miiko na kusimamia maadili ya taaluma,aliziomba taasisi zinazowatumia kuzingatia usalama wao na kuwapa vyombo bora vya usafiri.