Na Sophia Kingimali.
Shirika la Msichana Initiative kupitia mradi wake wa Sauti yangu Nguvu yangu imetoa rai kwa serikali kuanzia ngazi ya mitaa,vijiji mpaka kata kuwapa ushirikiano viongozi wawakilishi wao katika ngazi hizo pindi wanapotoa elimu kwa umma ili kuibua changamoto zinazowakabili watoto na wanawake ikiwemo ukatili.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 23,jijini Dar es salaam msimamizi wa mradi huo Rosemarry Richard wakati wa kikao na viongozi wa mikoa minne ili kujadiliana namna ya msichana anavyoweza kubeba agenda yake pamoja na kujipigania.
Amesema uwepo wa mafunzo hayo ni kuendelea kuzalisha wasichana watakaoweza kusimama katika harakati na kuzibeba agenda zao na kuzisimami.
Amesema uwepo wa viongozi hao vijana katika ngazi mbambali katika jamii unasaidia kutoa elimu ya kupinga ndoa za utotoni,kuhamasisha kuhusiana na usawa wa kijinsia lakini kuleta chachu ya uongozi kwa wanawake.
“Kupitia viongozi hawa 20 kutoka mikoa minne wameweza kuunda vikundi ambavyo vimefikia wasichana 240 lakini pia kuibua kesi 5 za ndoa za utotoni”amesema.
Aidha Rosemarry ameongeza kuwa lengo la kuendelea kutoa elimu kwa wasichana ni kuendelea kuzalisha wanaharakati ambao wataweza kusimama kujitetea lakini pia kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi chini mpaka serikali kuu.
Kwa upande wake leonardina Sosthenes Msichana kiongozi kutoa mkoa wa pwani wilaya ya Bagamoyo amesema katika mkoa huo kumekuwa na wimbi kubwa la ndoa za utotoni ambapo chanzo kikibwa ni tamaa za mali na kukosekana kwa elimu ya ukatili kwa watoto.
Amesema kupitia shirika la msichana wameweza kuokoa watoto watatu ambao waliingia kwenye ndoa na kufanikiwa kuwarudisha shule.
“Suala la ndoa za utotoni likekuwa changamoto sana katika mkoa wetu tumeokoa watoto watatu ambao waliolewa kwenye umri mdogo na tumewarudisha shule kuna mmoja yeye alikua mjamzito tulimsaidi akafanya mitihani ya darasa la saba,amejifungua disemba na sasa yupo kidato cha kwanza”Amesema.
Naye,msichana kiongozi Mwajuma Hima kutoka wilaya ya Ubungo ametoa rai kwa wazazi kuwa karibu na watoto na kutokuwaamini ndugu na kuwaachia watoto kwani wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa ukatili kwa watoto.