Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka wa Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya hali ya hewa, Dkt. Ladislaus Chang’a akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 22/02/2024 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa rasmi ya utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2024 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka.
………….
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2024 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 22/02/2024 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya hali ya hewa, Dkt. Ladislaus Chang’a amesema kuwa maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
“Mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi, Mvua hizi zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Februari katika maeneo mengi na kuisha wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Mei 2024, Aidha, aliongeza kuwa ongezeko la mvua linatarajiwa katika kipindi cha mwezi Machi 2024.” amesema Dkt. Chang’a.
Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Chang’a amesema kuwa vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza hivyo kuweza kusababisha mafuriko, milipuko ya magonjwa pamoja na athari nyingine zitokanazo na mvua nyingi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Chang’a ameshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya uangazi wa hali ya hewa na hivyo kuiwezesha TMA kufikia hatua ya kuongeza usahihi wa utabiri.
Dkt. Chang’a amesisitiza jamii kuendelea kufuatilia taarifa za mara kwa mara zinazotolewa na TMA kwa vile ni za uhakika, huku akibainisha kuwa usahihi wa msimu wa Vuli 2023 ulikuwa asilimia 98.