Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akikagua daraja la muda la Mirumba lililopo katika jimbo la Kavuu tarehe 22 Februari 2024.
Mbunge wa jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akipata maelezo ya maandalizi ya ujenzi wa daraja la Mirumba tarehe 22 Februari 2024.
Mbunge wa jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akikagua maandalizi ya ujenzi wa daraja la Mirumba lililopo halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi wakati alipofanya ziara kwenye eneo hilo tarehe 22 Februari 2024.
Muonekano wa daraja la muda la Mirumba lililopo halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.
Mbunge wa jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akizungumza na waendesha bodaboda alipowatembelea katika vijiwe mbalimbali katika jimbo lake la Kavuu kwa lengo la kujua changamoto zao 22Februari 2024.
………….
Na Munir Shemweta, KATAVI.
Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amekagua daraja la muda pamoja na maandalizi ya ujenzi wa daraja la Mirumba lililopo kwenye jimbo lake katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.
Daraja hilo linaunganisha mkoa wa Katavi na Rukwa lina urefu wa mita 60 na litagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 6.55.
Mhe. Pinda amekagua daraja hilo tarehe 22 Februari 2024 katika kata ya Mirumba ikiwa ni muendelezo wa kukagua shughuli za maendeleo katika jimbo lake sambamba na maandalizi ya mkutano Mkuu wa jimbo hilo unaotarajiwa kufanyika februari 24, 2024.
Akiwa katika eneo la daraja hilo, Mhe. Pinda ameoneshwa kuridhishwa na ujenzi wa daraja la muda pamoja na maandalizi ya lile la kudumu na kueleza kuwa, daraja hilo litakuwa suluhisho ya shida ya muda mrefu ya wananchi wa Mirumba waliyokuwa wakiipata wakati wa mvua kubwa.
Mbunge huyo wa Kavuu amesema, anamuamini mkandarasi aliyepewa kazi ya ujenzi wa daraja kutokana na kufanya kazi nzuri ya ujenzi wa daraja la Mwamapuli-Chamalendi alilolieleza kuwa lina kiwango bora na sasa limeanza kutumika.
‘’Mkandarasi! mimi sina tatizo na wewe na nina imani kazii hii ya ujenzi wa daraja la Mirumba itafanyika vizuri na kwa ufanisi, nikutakie kila la kheri’’ alisema Mhe. Pinda.
Utekelezaji ujenzi wa daraja la Mirumba unafanywa na kampuni ya ujenzi ya Safari General Business Co Ltd JV Advance na ni wa miezi 24.
Katika hatua nyingine Mbunge huyo wa jimbo la Kavuu aliwatembelea vijiwe vya waendesha boda boda kwa lengo la kujua changamoto zinazowakabili wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Akiwa katika vijiwa hivyo, Mhe. Pinda aliwataka waendesha boda boda kuwa makini wakati wote wanapofanya kazi zao kwa kuwa umakini ndiyo utakaowawezesha kuepukana na ajali zinazoweza kuepukika.
Aidha, Mbunge huyo wa Jimbo la Kavuu amewaahidi waendesha bodaboda wa vijiwe vyote vya jimbo lake kuwapatia vizibao (Reflector) ili wavivae wakati wote wanapofanya kazi zao.
Kwa upande wao, waendesha boda boda mbali na kumshukuru Mbunge wa kwa uamuzi wa kuwapatia Reflector walimuomba aangalie uewezekano wa kuwasaidia kupata mikopo ya pikipiki kutoka kwa kampuni zinazouza pikipiki. Mhe Pinda aliahidi kulifanyia kazi suala hilo.