Waziri wa Nchi (OR) Katiba ,Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe.Haroun Ali Suleiman akizungumza na walimu wa madrasa wakati akifunga ya mafunzo ya walimu hao mkupuo wa kwanza huko skuli ya Amali Kiongoni Makunduchi Wilaya ya kusini Mkoa wa Kusini Unguja .
Waziri wa Nchi (OR) Katiba ,Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe.Haroun Ali Suleiman akimkabidhi cheti miongoni mwa wahitimu wa mafunzo ya walimu wa madrasa mkupuo wa kwanza huko skuli ya Amali Kiongoni Makunduchi Wilaya ya kusini Mkoa wa Kusini Unguja .
Katibu Mtendaji Ofisi ya mufti Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume akizungumza katika hafla ya ufungaji wa mafunzo ya walimu wa madrasa mkupuo wa kwanza huko skuli ya Amali Kiongoni Makunduchi Wilaya ya kusini Mkoa wa Kusini Unguja.
NA SABIHA KHAMIS, MAELEZO
Waziri wa Nchi OR Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala bora, Mhe. Haruna Ali Suleiman amewataka walimu wa madrasa kuitumia vyema elimu waliopatiwa ili kuboresha maadili ya watoto na kupata Taifa lililobora.
Akizungumza wakati akifunga mafunzo ya walimu wa madrasa mkupuo wa kwanza kwa Wilaya ya Kusini, huko katika skuli ya Amali Kiongoni Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja amesema endapo mafunzo hayo yatatumika ipasavyo yataenda kubadilisha maisha ya wanafunzi hao.
Aidha aliitaka ofisi ya mufti kuyaendeleza hayo mafunzo hadi kufikia ngazi mbalimbali ili wanafunzi wa madrasa wapate elimu bora inayoendana na wakati.
Hata hivyo alifahamisha kuwa kutokana na masomo waliyopatiwa walimu hao yatawasaidia kupata ujuzi na kujua njia bora za kujifunza na kufundishia, pamoja na kubadilisha dhana ya ufundishaji madrasa kiujumla .
Kwa upande wake Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume amewataka walimu wa madrasa kuwasimamia vyema wanafunzi na kuondoa mianya yote inayopelekea kutokea kwa vitendo vya udhalilishaji.
Amesema endapo madrasa hazitakua na uwiyano wa walimu wa kike na wakiume na kuwakusanya wanafunzi nyakati za usiku vitendo vya udhalilishaji vinaweza kutokezeaa.
Aidha aliwaomba walimu wa kiume kuacha kukaa faragha na wanafunzi wa jinsia moja au tofauti kwani ni miongoni mwa vichochezi vya vitendo hivyo.
Sheikh khalid alifahamisha kuwa mafunzo hayo ni ya mezi mitatu na masomo mbalimbali walipatiwa walimu hao ikiwemo lugha ya kiarabu na kiengereza, pamoja na saikolojia ili kutambua hitaji la mwanafunzi na jinsi ya kumsaidia.
Hata hivyo alisema mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo walimu wa madrasa juu ya mbinu mpya za kufundishia wanafunzi wa madrasa ili kuinua ufahamu wao.
Nao wahitimu wameahidi kuyafanyia kazi ipasavyo mafunzo hayo pamoja na kuzitumia mbinu mbalimbali walizopatiwa ili kuimarisha elimu ya madrasa kwa wanafunzi.
Pamoja na hayo wameahidi kushirikiana kwa pamoja ili kuunda jumuiya itakayoweza kuhamasisha jamii ili kuinua hadhi ya walimu wa madrasa.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Ofisi ya Mufti Zanzibar na Jumla ya wanafunzi 70 wamehitimu mafunzo ya walimu wa madrasa na kukabidhiwa vyeti pamoja na leseni za kusomesha madrasa.