Ofisa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Reuben Magandi, alipokuwa akizungmza waandishi wa habari (hawapo pichani)
Dkt. Elikana Kalumanga, Meneja Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi wa Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili akifafanua jambo kwa washiriki wa semina.
Dastan Kamanzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF)
…………………….
NA SIDI MGUMIA, BAGAMOYO
Umasikini, kipato duni vyatajwa kuwa ni moja ya sababu kubwa za wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi nchini.
Hayo ni kwa mujibu wa Ofisa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Reuben Magandi, alipokuwa akizungumza hivi karibuni wakati wa semina ya siku mbili ya waandishi wa habari za mazingira iliyofanyika wilayani Bagamoyo na kuratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kupitia mradi wake wa USAID Tuhifadhi Maliasili.
Magandi amesema mojawapo ya vitu ambavyo vinasababisha uvamizi katika hifadhi za misitu ni umasikini ambapo mtu anaona kuwa ni njia rahisi zaidi ya kujipatia kipato.
“Sababu kubwa inayosababisha wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi za misitu na kufanya ushughuli kama uchomaji mkaa, upasuaji mbao na nyingine ni umasikini ambapo mtu anaona kuwa ni njia rahisi zaidi ya kujipatia kipato,” amesema Magandi.
Amesema vitendo hivyo vya uvamizi wa maeneo hayo kwa shughughuli kama kilimo, uchomaji mkaa na upasuaji wa mbao imekuwa ni changamoto kubwa inayorudisha nyuma juhudi za TFS huku akitaja chanzo kuwa ni hali ngumu ya maisha.
Magandi anasema kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo wamekuwa wakizishirikisha jamii zinazozunguka misitu kupata njia mbadala ya kujipatia kipato.
“Tumekuwa tukiwawezesha kwa kuwapatia mbinu mbadala za kujipatia kipato ambapo ni pamoja na kuwagawia miche ya miti ikiwamo ya matunda kwa jamii zote zinazozunguka misitu asili.
“Pia tumekuwa tukiwapa mizinga kwa ajili ya ufugaji nyuki, mbinu hizi zote zinawasaidia wananchi kujipatia kipato pamoja na kutunza mazingira badala ya kukata miti kwa ajili ya mbao na mkaa, hivyo hii inakuwa inawahamasisha zaidi wao kuwa walinzi wa mazingira badala ya kuharibu,” anasema Magandi.
Aidha amefafanua kuwa miti ya asili inayosimamiwa na TFS inaendelea vizuri isipokuwa maeneo ambayo yana uvunaji mkaa.
“Maeneo ambayo bado yanachangamoto ni yale ambayo kuna uvunaji wa mkaa, hivyo TFS tunajitahidi kuhakisha kuwa uoto huo ulioharibika unarudishiwa kwa kushirikiana na wananchi,” anasema.
Naye Meneja Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi wa Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Dkt. Elikana Kalumanga amesema kasi ya uharibifu wa mazingira kwa kukata miti, uharibufu wa vyanzo vya maji na uzalishaji wa hewa ukaa ni kubwa ndani na nje ya Tanzania hali inayofifisha uwezekano wa kuyarejesha katika uhalisia wake wa kawaida kwa haraka kama ilivyokuwa ikifanyika miaka mingi iliyopita.
Dkt. Kalumanga, amesema suala la uharibifu wa mazingira yaliyochangia mabadiliko ya tabia yameanza miaka milioni 445 iliyopita, hata hivyo haikuwa rahisi athari zake kuonekana kwa haraka kutokana na kasi yake kuwa ndogo.
“Suala la uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi, hayakuanza leo, yalianza miaka milioni 445 iliyopita na katika nyakati hizi yalikuwa yakichangiwa zaidi na mambo ya asili na mazingira yalikuwa yanaweza kujirejesha yenyewe katika hali yake ya kawaida.
“Kwa sasa hali ni tofauti, mapinduzi ya teknolojia na kuongezeka kwa shughuli za kibidanamu kumekuwa ni tatizo kubwa na kama hakutakuwa na jitihada za makusudi za kuyarejesha mazingira kwenye asili yake ni wazi hali itakuwa mbaya zaidi miaka ijayo,” amesema Dkt. Kalimanga.
Wakitoa darasa kwa waandishi wa habari za mazingira juu ya namna sahihi ya kuandika habari za mazingira, Dastan Kamanzi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) na Pili Mtambalike ambaye ni Mkufunzi na Mshauri wa Masuala ya Habari nchini, wamesema habari za uhifadhi zina tija kubwa kwa nchi na ni jukumu la waandishi kuhakikisha wanaandika makala nzuri ili zisaidie kuleta tija kwenye uhifadhi na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Waandishi wa Habari wakiondoka kwenye utamaduni wa kuandika habari nyepesi nyepesi na kujikita kwenye kundika habari zinazogusa maslahi ya jamii, ni wazi wao watakuwa chachu ya mabadiliko ya nchi na maisha yao kwa ujumla,” amesema Kamanzi
“Habari za uhifadhi zina tija kubwa kwa nchi na ni jukumu la waandishi wa habari za mazingira kuhakikisha wanaandika makala nzuri zilizojaa taarifa za kweli na takwimu sahihi ili zisaidie kuleta tija kwenye uhifadhi na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi,”amesema Mtambalike.
Akizungumzia mchango wa warsha hiyo ya siku mbili iliyoshirikisha waandishi wa habari 20 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo amebainisha kuwa ni sehemu ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID).
Hata hivyo Chikomo amesema kuwa ili kupunguza changamoto hizo, ni vyema waandishi wa habari wakaelimisha jamii kuhusu faida na hasara za utunzaji mazingira katika kulinda shoroba na misitu.
JET kwa kushirikiana na USAID wamekuwa wakiratibu mafunzo na kuwezesha waandishi kwenda kuona na kuandika habari za uhifadhi wa shoroba ambapo matokeo yake yamekuwa mazuri.
Chikomo amesema kuwa ni mwaka wa tatu tangu kuanza kwa uekelezaji wa mradi huo na kumekuwa na mafanikio, hivyo ni vyema waandishi wakendelea kuelimisha jamii kupitia kalamu zao ikiwa ni pamoja na kuongeza nguvu katika uandikaji habari kuhusu faida za utunzaji misitu.
Awali, akifungua mafunzo hayo, Mwenyekiti wa JET ,Dkt. Ellen Otaru alisema anaamini waandishi wa habari wanaouwezo mkubwa wa kuongeza ushawishi kwa wananchi, wadau na watoa maamuzi ili kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira na uhifadhi wa wanyama pori.
Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili umelenga kuujua umuhimu wa kuhifadhi mapito ya wanyamapori maarufu kama shoroba pia kupambana na uharibifu wa misitu, wanyamapori, mabadiliko ya Tabianchi na uhifadhi wa viumbe hai kwa ujumla wake.