……………..
Wizara ya Maliasili na Utalii imepongezwa kwa hatua inazoendelea kuzichukuwa katika uboreshaji wa usimamizi wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW)
Pongezi hizo zimetolewa na mtaalam na mwezeshaji wa Mafunzo ya Usimamizi wa vihatarishi kutoka Wizara ya Fedha Dkt. Sako Mayrick, katika ufunguji wa Mafunzo ya kuandaa rejista ya vihatarishi kwenye mradi wa REGROW yaliyotolewa kwa Maafisa wa Mradi huo, mkoani Morogoro
Dkt. Mayrick ameongeza kuwa maamuzi ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya kuwa na Mafunzo hayo ni kitendo cha kupongezwa na kuungwa mkono na miradi mingine ambayo haina rejista ya vihatarishi ili kuwezesha kutambua vihatarishi mbalimbali vitakavyo weza kukwamisha utekelezaji wa miradi hiyo.
Akifunga Mafunzo hayo, Msimamizi Mkuu wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) Dkt. Aenea Saanya, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo zaidi Maafisa wa mradi huo ngazi ya Wizara, wa kutambua viashiria hatarishi vinavyoweza kukwamisha shughuli za utekelezaji wa mradi.
Dkt. Saanya ameongeza kuwa mafunzo hayo yametoa matokeo chanya baada ya wataalam hao kuandaa mpango wa usimamizi na rejista ya vihatarishi katika kufikia malengo ya mradi wa REGROW.
Aidha Dkt. Saanya ameongeza kuwa, uongozi wa Mradi huo utaendelea kushirikiana na wadau na taasisi mbalimbali ili kupata mawazo na uzoefu zaidi kwa maslai mapana ya utekelezaji wa mradi wa REGROW.
Mradi wa REGROW wenye lengo la kuboresha usimamizi wa maliasili na kukuza utalii kusini mwa Tanzania unatekelezwa katika hifadhi za kipaumbele za Ruaha, Udzungwa, Mikumi na Nyerere na Hifadhi ya Msitu wa Asili Kilombero kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia.