………………
Rais mstaafu wa Msumbiji Mhe.Joachim Chisano ametembelea Makumbusho ya Taifa la Tanzania ambapo amepata fursa ya kujionea na kujifunza Urithi wa asili na Utamaduni wa Tanzania katika vituo vya Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni na Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo tarehe 21 Februari 2024 baada ya kutembelea vituo hivyo Rais Chisano amesema amevutiwa na namna ambavyo Makumbusho ya Taifa la Tanzania inavyohifadhi historia ya Tanzania kwa weledi mkubwa.
Aidha Rais mstaafu Chisano amesema ni vyema Makumbusho ikaendelea kuenzi lugha ya Kiswahili maradufu kwa kuitumia kwenye utekelezaji wa majukumu ya Uhifadhi wa historia na urithi wa asili.
“Tunaweza kuendeleza Lugha ya Kiswahili ikiwa ndio lugha ya maendeleo ya Afrika Mashariki, watu wanajifunza Kiingereza kwa shughuli nyingine lakini tunatamani na watu wengine wajifunze lugha zetu za Kiafrika, kitu cha muhimu ni kuendelea kufanya utafiti na uchunguzi akitolea mfano wa neno Kilimanjaro ambalo linapaswa kuelezewa kwa undani zaidi”amesema Rais mstaafu Chisano
Hata hivyo, Rais Mstaafu Chisano ameeleza kuvutiwa na namna Nyumba za asili za makabila ya Tanzania zilivyojengwa katika Kijiji Cha Makumbusho na kusema kuwa utamaduni wa Afrika hautofautiani sana kutoka nchi moja na nyingine.
“Nimefurahi sana kuja tena hapa Tanzania kuona utamaduni na maisha ya Watanzania, namna wanavyoishi majimbo mbalimbali na Makabila yao katika umoja huu, nimegundua pia mfanano wa tamaduni mbalimbali baina ya Tanzania na Msumbiji lakini pia katika nchi nyingine za Afrika nilizotembelea”Amesisitiza Mhe. Chisano.