Ashrack Miraji Same Kilimanjaro
Waziri wa maliasili na Utalii Mhe.Angellah Kairuki anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tamasha kubwa la Utalii la Same Utalii Festival lililoandaliwa na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Same kwa ushirikiano na wadau wengine likilenga kuibua na kutangaza maeneo mbalimbali yenye vivutio vya Utalii.
Akizungumza na waandishi wa habari juu ya maandalizi ya tamasha hilo, mkuu wa wilaya ya Same Kasilda Mgeni amesema kwa sehemu kubwa maandalizi yamekamilika matarajio ni kupokea wageni zaidi ya elfu mbili na tayari baadhi yao wameanza kuwasili.
“Mtakumbuka kuwa Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassani alifanya ile filamu ya Tanzania The Layal Tour kwa ajili ya kutangaza vivutio vya Utalii na sasa sisi kama ofisi ya mkuu wa wilaya ya Same tumeona tuendeleze kile alicho kianzisha Mhe.Rais ndipo kwa kushirikiana na wadau wengine tumekuja na tamasha hili la Same Utalii Festival ambalo litakuwa likifanyika kila mwaka”.Alisema mkuu huyo wa Wilaya.
Tamasha hilo linalokwenda na kauli mbiu isemayo Alianzisha Mama na sisi tunaendeleza limepangwa kufanyika kila mwaka ambapo mbali na kutangaza vivutio vya Utalii linalenga pia kuongeza fursa kwa wakazi wa Same ikiwemo ajira na uwekekezaji, kwakua limepangwa kuhudhuriwa na idadi kubwa ya watu wakiwemo wageni wanaotoka nje ya wilaya ikizingatiwa pia ni endelevu hufanyika kila mwaka.
Kwa upande wake Mkuu wa hifadhi ya Taifa mkomazi SAC.Emmanuel Moirana amesema hamasa inayofanywa na viongozi kutangaza utalii kwa kiasi kikubwa imesaidia kuongezeka kwa idadi ya wageni matharani tangu Filamu ya Tanzania The Layal Tour kumekua na ongezeko la wageni hasa wanaotoka mataifa mengine.
“Leo kuna wageni wameanza kuingia kwa ajili ya Same Utalii Festival na sisi hifadhi ya Taifa Mkoamazi tupo tayari kuhakikisha wageni wote wanafurahia mazingira na kujionea vivutio tulivyo navyo ikiwemo wanyama Adimu Faru Weusi ambao hawapatikani kwenye hifadhi nyingine”.Alisema Moirana mkuu wa hifadhi ya Taifa Mkomazi.