Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mheshimiwa January Makamba, anatarajiwa kushiriki katika Mkutano wa 9 wa RAISINA (9TH RAISINA Dialogue) unaotarajiwa kufanyika nchini India kuanzia Februari 21 hadi 23, 2024. Ushiriki wake katika mkutano huo unaonesha azma ya Tanzania katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, diplomasia na kutafuta ushirikiano wenye tija kwa maslahi mapana ya kiuchumi na kijamii ya Taifa.
Mkutano huo wa RAISINA unaofanyika kila mwaka unaandaliwa na Observer Research Foundation (ORF) ya India kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo tangu mwaka 2016. Mkutano huo unawakutanisha nguli wa wanadiplomasia, watunga sera, wasomi,waandishi wa habari, wafanyabiashara, wataalamu na wadau kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa lengo la kujadili na kutafuta majawabu ya changamoto za kiuchumi na kisiasa zinazo ikabili dunia.
Ushiriki wa Tanzania kwa mara ya kwanza katika mkutano huo tokea kuanzishwa kwake, kunashsiria azma ya serikali ya kutumia ushawishi wake wa kidiplomasia katika kutafuta fursa, kulinda na kutetea maslahi ya Tanzania kwa manufaa ya wananchi wake.
Kuongezeka kwa ushawishi wa Tanzania na kukubalika kwake katika majukwaa ya kimataifa pamoja na masuala mengine kunatokana na uongozi imara, amani na utulivu wa kiasiasa uliopo nchini, nafasi ya kimkakati ya kijiografia, uwingi wa rasilimali na ukuaji endelevu wa uchumi wa Nchi.
Bila shaka, ushiriki wa Makamba katika jukwaa hili la kimataifa unaakisi dhamira yake ya kuendeleza maslahi na diplomasia ya kimkakati ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa kwa kuendelea kuimarisha urafiki wa kudumu na mataifa mengine na taasisi za kimataifa.
Mbali na hayo Waziri Makamba katika mkutano huo anatarajiwa kuonyesha dhamira ya Tanzania ya kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kukuza biashara, vilevile kuonesha jitihada na hatua iliyofikiwa na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na changamoto zinazofifisha ukuaji wa sekta muhimu kama vile upatikanaji wa maji safi na salama, afya, mawasiliano, kilimo, nishati, uchumi wa buluu, kilimo na madini.
Jambo la muhimu zaidi mkutano huo unatoa fursa hadhimu kwa serikali ya Tanzania kushiriki moja kwa moja kwenye mazungumzo yenye tija katika uhusiano wa kidiplomasia na India na Nchi mbalimbali duniani. Hatua hiyo itachagiza ukuaji maradufu wa biashara, uwekezaji, teknolojia na na utalii na kuchangi katika ukuaji wa uchumi na kuongezeka kwa fursa za ajira ndani na nje ya nchi.
Tanzania na India zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu wa kiuchumi na kidiplomasia hususan katika biashara na uwekezaji ambao umeifanya India kuwa mshirika wa tatu mkubwa wa biashara wa Tanzania, ikikadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.1 kwa mwaka 2022/2023.
Kiasi hiki kimeendelea kukua ikilinganishwa na dola za Kimarekani bilioni 2.6 katika kipindi cha 2017-2018. Mwaka 2021/2022 India imerekodiwa kusajili miradi 630 ya uwekezaji nchini yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.7 ambayo imezalisha ajira zaidi 60,000.