Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewataka wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo na kata kufuata na kuzingatia sheria wakati wa kutelekeza majukumu yao ili uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 23 ufanyike kwa ufanisi na kupunguza au kuondoa malalamiko wakati wote wa uchaguzi.
Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Hahakama Kuu Mhe Asina Omari kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume, wakati akifungua mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi ngazi ya jimbo na kata zinazotarajia kufanya uchaguzi mdogo wa madiwani tarehe 20 Machi, 2024.
Amesema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kisheria ambazo hupaswa kufuatwa na kuzingatiwa kwani hatua na taratibu hizo ndio msingi wa uchaguzi kuwa mzuri na wenye ufanisi.
Mhe. Asina amewaasa wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo na kata wahakikishe wanazingatia maelekezo watakayopewa na Tume badala ya kusimamia uchaguzi kwa mazoea.
“Hata kama umeshasimamia chaguzi kadhaa hapo nyuma, lakini uchaguzi huu mdogo unaojumuisha kata 23 haujawahi kuusimamia. Baada ya mafunzo hayo ndipo mtaweza usimamizi, Hivyo uzoefu wenu mkautumie kuhakikisha uchaguzi huu unafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu”, alisema Mhe. Asina.
Aliwasisitiza watendaji hao kuwa wakati wote wa mchakato wa uchaguzi, wavishirikishe vyama vya siasa na wadau wengne wa uchaguzi katika maeneo yao kuhusu masuala ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa kwani jambo hilo litawarahisishia utekelezaji wa majukumu yao.
Mhe. Asina aliwakumbusha wasimamizi hao kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo husika kwa lengo la kuhakikisha mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.
“Nawasisitiza kuhakikisha mnaajiri watendaji wa vituo wenye weledi, wanaojitambua na tuachane na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi na kuhakiki vifaa vya uchaguzi mnavyopokea kutoka Tume na kuhakikisha kila mkuu wa kituo anapata vifaa vyote vya uchaguzi vinavyohitajika mapema”, alisema Mhe. Asina.
Aliwataka wasimamizi hao kuvipatia vyama vya siasa orodha ya vituo vya kupigia kura ili kuviwezesha kupanga mawakala na kuhakikisha siku ya uchaguzi wanaweka utaratibu utakaowezesha kila kituo cha kupigia kura kufunguliwa saa 1:00 asubuhi.
Mafunzo haya kwa wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo na kata yana lengo la kuwajengea uwezo, kuwakumbusha wajibu na majukumu yao wasimamizi hao na kupata fursa ya kujadiliana namna ya kufanikisha uchaguzi na kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.