Na John Mapepele
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki amewataka wadau wote kwenye mnyororo zao la mianzi kushirikiana na Serikali ili kuleta mapinduzi katika kuzalisha kwa wingi hatimaye kuchangia kwenye uchumi na tabianchi huku akisisitiza kuwa tumechelewa.
Mhe. Kairuki ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam alipoambatana na katibu Mkuu wa Wizara yake Dkt. Hassan Abbas, kwenye kikao cha ufunguzi wa Mkakati wa Mianzi pamoja na Mpango Kazi wake wa kipindi cha Mwaka 2021-2031 uliobeba Kauli mbiu ya ‘Tanzania inawekeza kwenye mianzi kwa ajili ya uhimilivu na kwa uchumi endelevu.
„Ndugu zangu mtakumbuka Tanzania ni miongoni mwa nchi wajumbe waanzilishi wa Shirika la Mianzi Duniani (INBAR) na nchi ya kwanza kabisa kutoka bara la Afrika wakati INBAR linaanzishwa mwaka mwaka 1997 leo tunapozindua mkakati huu tunatakiwa kutambua kuwa tumechelewa tunatakiwa kupiga hatua kwa wadau wote kushiriki kikaamilifu katika kutekeleza kulingana na Sheria, Kanuni na Miongozo ambayo ipo.” Amesisitiza Mhe. Kairuki
Amesema uzinduzi wa mkakati huo ni fursa adhimu kwa Sekta Binafsi, Makampuni, Mashirika na Wawekezaji kushiriki kikamilifu katika kuleta mapinduzi ya kilimo cha mianzi ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na malighafi ya kutosha ya kuweza kuendesha viwanda vya kuchakata mianzi na huku nchi ikiuza hewa ya ukaa kwa ajili ya kuongeza pato la Taifa na mtu mmoja mmoja.
Amesema matarajio ya Serikali ni kuwa, iwapo Mpango Kazi huo utatekelezwa ipasavyo utawezesha kuendeleza uhifadhi na matumizi endelevu ya misitu ya zao la mianzi kwa maendeleo endelevu katika sekta nyingine.
Aidha, Mhe. Kairuki ameielekeza Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha mbegu bora za mianzi zinapatikana kwa urahisi ili wananchi na wadau mbalimbali waweze kuzipata na kupanda pia kuwasaidia wananchi katika kuwapa elimu ya zao hilo kama wanavyofanya kwa mazao mengine ya misitu.
Pia ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) kufanya utafiti mara moja wa maeneo ambayo yanafaa kwa ajili ya zao ili yatumike kwa kilimo cha zao hilo.
Kwa upande wa Idara ya Misitu na Nyuki Waziri Kairuki ameiagiza kuandaa mara moja toleo jepesi la Mpango huo na kusambaza kwa wadau na wananchi ili waweze kutambua umuhimu na faida ya zao hilo tofauti na sasa ambapo mpango huo upo kwa lugha ya kiingereza.
„Ninaielekeza Taasisi ya Utafiti wa Misitu kufanya tafiti za kutambua maeneo sahihi ya kupanda aina mbalimbali za mianzi pamoja na kuiagiza Idara ya Misitu na Nyuki ifanye tafsiri ya nyaraka hizi mbili kwa lugha ya Kiswahili na kuzisambaza. Serikali itaweka mazingira wezeshi kwa wadau wote wa zao la mianzi ili kuhakikisha linaleta tija kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla.” Ameongeza, Mhe Kairuki
Waziri Kairuki pia amekielekeza Chuo Cha Viwanda vya Misitu Moshi kwa kushirikiana na SIDO na wadau wengine washirikishwe kutafuta teknolojia za kisasa za kuchakata mazao ya mianzi ili kuyaongezea mnyororo wa thamani na kupata fedha nyingi kwa kuuza mazao hayo ndani na nje ya nchi.
Vilevile ameutaka Mfuko wa Misitu nchini kuweka vipaombele vya utekelezaji wa mpango huo kwenye bajeti zake za kila siku huku akisisitiza wadau kuendelea kumuunga mkono kwenye juhudi za uhifadhi wa mazingira hususan misitu unaolinufaisha Taifa kwa sasa na vizazi vijavyo kupitia fursa mbalimbali ikiwemo hewa ya ukaa.
“Hivyo, nitoe wito kwa Wadau wote kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi shupavu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kuwaletea maendeleo Wananchi na kuhifadhi mazingira.”
Shirika la Mianzi Duniani (INBAR) hapa nchini Mhe. Balozi Ali Mchomo ameiomba Serikali kuendelea kutoa elimu ya zao la mianzi kwa wananchi huku akisisitiza serikali kuwahama wadau mbalimbali waweze kuwekeza katika mnyororo wa thamani wa zao hilo.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ikiongozwa na Mwenyekiti wake Timotheo Mzava, viongozi wa Serikali kutoka mikoa na taasisi mbalimbali, wafadhiri pia mashirika binafsi ambapo pia Mhe. Kairuki alipata fursa ya kukagua maonesho maalum ya zao la Mianzi.