Na Mwandishi wetu, Nzega
MKUU wa Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, Naitapwaki Tukai, tangu mwaka 2023 hadi hivi sasa 2024 ameliongoza eneo hilo kwa ufanishi mkubwa huku akisimamia maendeleo mbalimbali na kuongoza vyema watu wa eneo hilo.
Wilaya ya Nzega ni miongoni mwa Wilaya kongwe nchini yenye Halmashauri mbili na Majimbo matatu ya Nzega Mjini inayoongozwa na mbunge wake, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, Nzega Vijijini ya mbunge Dkt Hamis Andrea Kigwangalah na Bukene ya mbunge Suleiman Zed.
DC Tukai pamoja na kuongoza ipasavyo Wilaya hiyo ameweza kuyaunganisha makundi mbalimbali ikiwemo madereva wanaobeba abiria maarufu kama (bodaboda), wakulima, wafugaji, wamachinga, wafanyabiashara na wazee wa eneo hilo.
Amesimamia vyema ujenzi wa zahanati kwenye vijiji na vituo vipya vya afya kwenye kata na tarafa, katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri mbili na majimbo matatu yaliyopo kwenye Wilaya ya Nzega na jamii kupata huduma za afya.
Pia, amehakikisha fedha zote zilizotengwa kwenye ujenzi wa madarasa ya shule mpya za msingi na sekondari, ofisi na nyumba mpya za walimu zinakamilika ujenzi wake.
Kwenye miradi mipya ya maji na barabara, mkuu huyo wa wilaya amehakikisha imekamilika na kunufaisha wananchi wa Nzega hivyo kufanikisha maendeleo.
Hata viongozi wa dini zote wameona utofauti mkubwa kwa DC huyu kwani amekuwa akishirikisha madhehebu yote kuwa wamoja kwa waislamu na wakristo amewaweka viongozi wa dini kuwa rafiki zake wa karibu katika kufanikisha umoja wao unaleta maendeleo.
Sheikhe wa Wilaya hiyo Zahoro na Mwenyekiti wa makanisa ya CCT Mchungaji Magambo wanao ushuhuda juu ya DC Tukai alivyoleta mabadiliko.
Akizungumza baada ya kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wake wilayani Nzega, DC Tukai amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa na heshima aliyompatia ya kumwakilisha katika kipande hicho cha Nzega.
“Namshukuru Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Mheshimiwa Batilda Salha Buriani kwa kutuongoza vyema nawashukuru pia viongozi mbalimbali wa chama na serikali Wilaya ya Nzega, nawashukuru mno kwa ushirikiano mnaonipa,” amesema DC Tukai.
Pia, amewashukuru watumishi wa ofisi yake kuanzia Katibu Tawala wa Wilaya, Kamati ya usalama ya Wilaya, Viongozi wa CCM wa Wilaya, maofisa Tarafa, watendaji wa kata, vijijini, vitongoji na mitaa na wananchi wote.
Amewashukuru wakurugenzi wa halmashauri zote mbili, Mwenyekiti wa Halmashauri, madiwani na watumishi wote wa halmashauri na ofisi yake kwa ushirikiano mkubwa waliompatia kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Mkazi wa Nzega mjini Thabiti Hassan amempongeza DC Tukai kwa namna anavyowaongoza wananchi wa eneo hilo bila kuwepo na matabaka.
“Mheshimiwa DC huyu kwa mwaka mmoja aliotuongoza ametuunganisha watu wa Nzega na kufanikisha maendeleo katika sekta mbalimbali,” amesema.