Na Mwandishi wetu, Simanjiro
DIWANI wa Kata ya Langai, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Jackson Leskar Sipitieck (Mugabe) amejitolea kumlipa shilingi 100,000 mwalimu wa shule ya msingi Langai ambaye anafundisha kwa kujitolea.
Pia Diwani huyo Sipitieck maarufu kama Mugabe, ametoa trekta lake na kuwalimia ekari 10 kwenye shamba la shule ili wanafunzi wa shule hiyo ya msingi Langai wapate kula chakula cha mchana shuleni.
Sipitieck akizungumza kwenye kikao cha kamati ya shule ya msingi Langai, amesema analipa shilingi laki moja kwa mwalimu huyo, lengo likiwa kumuwezesha mwalimu huyo anayejitolea kufundisha shuleni hapo.
“Baada ya kusikia changamoto ya mwalimu ambaye hajaajiriwa na Serikali anayejitolea kufundisha watoto wetu, nikaona niwezeshe hilo ili kumpa motisha ya kufundisha zaidi,” amesema Sipitieck.
Pia, amesema amejitolea kwa kutumia trekta lake na kulima ekari 10 za shamba la shule ya msingi Langai, kwa ajili ya chakula cha mchana kwa wanafunzi.
“Watoto wengi wanatembea umbali mrefu kutoka nyumbani hadi shuleni hivyo wasipokuwa na chakula shuleni hawataweza kusoma vyema na kufaulu,” amesema Sipitieck.
Mkazi wa kijiji hicho Alais Moringe amempongeza Diwani huyo kwa kujitolea misaada hiyo kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wa shule ya msingi Langai wanasoma kwa bidii.
“Mheshimiwa Mugabe ni mtu wa maendeleo kwani ameona uchungu mwalimu wa kujitolea kuishi kwenye changamoto ya malipo ndipo akaamua kumsaidia na pia kuwalimia watoto ili wapate chakula,” amesema Moringe.
Amewataka wakazi wa Kata ya Langai kumpa ushirikiano wa kutosha Diwani wao Sipitieck ili aweze kusimamia maendeleo na wao waone fahari ya kuwepo Simanjiro.
Amesema kumpata Diwani mwenye kudhubutu wa kujitolea kama huyo siyo jambo rahisi hivyo wanapaswa kumuunga mkono ili afanye maendeleo mengine zaidi.