Mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya Lindi mkoani Lindi Erieth Kalua kulia,akimsikiliza Mhandisi wa maji wa kanisa Anglikana Doyasisi ya Masasi Olaph John,wakati wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Lindi walipotembelea miradi ya maji katika kata ya Mandwanga na Mnara inayotekelezwa na Doyasisi hiyo kwa kushirikiana na shirika la World Vision Tanzania.
Mhandisi wa maji wa Kanisa Anglikana Doyasisi ya Masasi Olaph John,akimuonesha Mjumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Lindi ambaye ni mwakilishi wa mkuu wa wilaya hiyo Erieth Kalua namna mfumo wa umeme jua na umeme wa Tanesco utakavyotumika katika mradi wa maji wa Chiuta-Mikongi unaotekelezwa na Doyasisi hiyo.
Mhandisi wa maji wa Kanisa Anglikana Doyasisi ya Masasi Olaph John,akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi wa maji Mandwanga unaotekelezwa na Doyasisi hiyo kwa wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Lindi(hawapo pichani) waliotembelea ujenzi wa miradi ya maji katika kata ya Mandwanga na Mnara,wa pili kulia kaimu Askofu wa Kanisa Anglikana Doyasisi ya Masasi Douglas Msigala na wa kwanza kushoto Katibu Mtendaji wa Doyasisi hiyo Joyce Liundi.
………..
Na Mwandishi maalum, Mtama
WANANCHI wa kijiji cha Mandwanga na Lindwandwali Halmashauri ya wilaya Mtama wilayani Lindi,wamelishukuru Kanisa Anglikana Doyasisi ya Masasi kwa kuwajengea mradi mkubwa wa maji ya bomba utakaowaondolea adha ya muda mrefu ya ukosefu wa huduma ya maji safi na Salama.
Wametoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti mbele ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Lindi, waliotembelea mradi huo unaotekelezwa na kanisa Anglikana Doyasisi ya Masasi kwa kushirikiana na shirika la World Vision Tanzania,shirika la Grille Foundation na serikali ya Tanzania kupitia mradi wa maji na usafi wa mazingira.
Walisema,wana matumaini makubwa mradi huo utakapokamilika utawezesha kuondokana adha ya kutembea zaidi ya kilomita 5 kila siku kwenda kutafuta maji kwenye vyanzo vya asili na wengine kwenda vijiji vya jirani kuchota maji.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mwandwanga Lukia Issa alisema,awali katika kijiji hicho kulikuwa na mradi wa maji uliojengwa na taasisi moja ya dini,lakini umekufa kutokana na kukosa usimamizi wa karibu na baadhi ya miundombinu yake kuchakaa kwa sababu ya kukosa kufanyiwa ukarabati wa mara kwa mara.
Alisema,tangu wakati huo wamekuwa wakiteseka kwa kutumia maji ya visima yanayopatikana mbali na makazi yao, jambo linalosababisha kukosa kabisa muda wa kufanya shughuli nyingine za kiuchumi,hivyo kuongezeka kwa hali ya umaskini kwa wananchi.
Mkazi wa kijiji cha Lindwandwali Athuman Jawadu alisema,ujenzi wa mradi huo ni ukombozi mkubwa kiuchumi kwa sababu watapata nafasi ya kushiriki kazi mbalimbali za maendeleo ikiwemo kilimo,ufugaji na kufanya biashara ndogo ndogo zitakazowaingizia kipato badala ya muda huo kuutumia kwenda kutafuta maji.
Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Lindi Erieth Kalua,amelipongeza Kanisa Anglikana kwa kazi nzuri inayofanya ya kuisaidia serikali katika kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wa wilaya ya Lindi.
Kalua,amewataka wananchi wa vijiji vitakavyopitiwa na mradi huo kuhakikisha wanavuta maji majumbani,wanajenga vyoo bora ,wanalinda miundombinu ya mradi na kutumia maji hayo katika shughuli maendeleo ili kujiongezea kipato.
Kwa upande wake Msaidizi wa Askofu wa kanisa Anglikana Doyasisi ya Masasi Douglas Msigala alisema,kanisa hilo litaendelea kushirikina na kuisaidia serikali katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo hasa katika suala zima la kuimarisha na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.
Amewashukuru wananchi wa kata ya Mandwanga,kwa kutoa maeneo yao bure kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na miradi ya maji ambayo itawawezesha wao wenyewe kupata huduma ya maji safi na salama na kanisa kungana mkono jitihada za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kumtua mama ndoo kichwani.
Alisema kazi ya kanisa siyo kuhubiri Injili tu,bali lina wajibu wa kuisaidia jamii kupitia watu wake bila kujali tofauti za dini,rangi wala kabila kuhakikisha wanapata huduma muhimu ilikupata waumini wenye afya njema watakaokuwa na uwezo wa kumtumikia Mungu wakati wote.
Hata hivyo,ameiomba serikali kupitia watendaji wa vijiji,kata na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kuanza kazi ya kuhamasisha wananchi kuingiza maji ya bomba kwenye nyumba zao badala ya kutumia vituo maalum vya kuchotea maji(vizimba).
Naye Mhandisi wa maji wa Doyasisi hiyo Olaph John alisema,mradi wa maji Mandwanga(Mandwangwa corridor) ulianza kujengwa mwaka 2022 kwa kuboresha kisima cha maji kilichochimbwa na serikali tangu mwaka 2009.
Alisema,kazi ya kwanza iliyofanyika ni kupima uwezo wake na kukifanyia usafi na baadaye kuanza kazi ya ujenzi wa uzio,kujenga nyumba ya mashine(Pump House,kufunga nishati ya umeme wa jua na kujenga matenki mawili,moja lenye uwezo wa kuhifadhi lita 50,000 katika kijiji cha Mandwanga na lingine la lita 35,000 kijiji cha Lindwandwali.
Mhandisi John alitaja kazi zilizofanyika hadi sasa ni kuchimba mitaro na kulaza mabomba umbali wa kilomita 11.5,kujenga vituo 12 vya kuchotea maji ambavyo vitakuwa kwenye mfumo wa Pre Paid ili kudhibiti mapato na upotevu wa maji.
Kwa mujibu wa John,mradi huo umesanifiwa kuhudumia wakazi zaidi ya 4,500 katika kijiji cha Mandwanga na zaidi ya 859 katika kijiji cha Lindwandwali na unauwezo wa kutoa huduma ya maji takribani kwa miaka 10 ijayo na unatekelezwa kwa gharama ya Sh milioni 552.