Na Ashrack Miraji Same
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro Azza Karisha amehitimisha mashindano ya Samia Cup yaliyokuwa yanachezwa kwenye Tarafa Ndungu katika jimbo la Same Mashariki.
Mashindano hayo yaliandaliwa na Mbunge wa jimbo hilo Anne Kilango Malechela yenye lengo la kuhamasisha michezo sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akihamasisha michezo kwa vitendo.
Mashindano hayo yamehitimishwa kwa mchezo wa fainali kuzikutanisha timu ya Boda boda FC kutoka kata Ndungu na Bendera FC kutoka Kata ya Bendera Vuje FC kutoka kata Vuje ambapo timu ya Bendera FC iliibuka mshindi kwenye fainali hiyo na kutangazwa kuwa Mabingwa wapya.
Akizungumza wakati akihitimisha michuano hiyo ya Samia Cup, Mwenyekiti huyo wa UVCCM amemshukuru Anne Kilango kwa kuamua kuanzisha mashindano ikiwa ni Sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Amesema mashindano hayo yamekuwa na tija kubwa kwa vijana kwa maana ya kujenga umoja, upendo, mshikamano pamoja na kuimarisha afya zao.
“Niendelee kumshukuru na kumpongeza Mwenyekiti wetu wa Chama Taifa ambaye ndiye Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa namna ambavyo amewajali wananchi wa tarafa ya Gonja kwa kuwaletea fedha nyingi za maendeleo katika sekta mbalimbali, ” amesema Karisha.
Pia amewaomba wananchi wa Ndungu kuendelea kumuunga Mkono Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mbuge wa jimbo la Same Mashariki Anne Kilango na CCM kwani ndicho Chama pekee kinachoweza kuwaletea wananchi maendeleo.
Aidha katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo ameongoza upandaji miti kwenye shule ya Msingi kamavmwendelezo wa utekelezaji wa kampeni ya Utunzaji wa Mazingira na kuifanya Same iwe ya kijani.
Kwa upande wake Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki amesema jimbo hilo lina tarafa tatu na tarafa zote wamemaliza mashindano hayo kila tarafa imetoa washindi watatu
Ameongeza baada ya hapo watapata timu tisa ambazo zitaunda tena mashindo ya Samia Cup washindi wa tatu wanaopatikana kwa kila tarafa watapatiwa zawadi baada ya mashindano hayo kukamilika na kumpata mshindi wa jimbo wa ligi ya Samia Cup.