Na Sophia Kingimali
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amewaasa wananchi kumuenzi hayati Edward Ngoyai Lowassa kwa kufanyakazi kwa bidii na kuyaishi yote mazuri aliyoyafanya katika kipindi chake cha utumishi.
Hayo ameyasema leo Februari 17,2024 wakati akiongoza mazishi ya Lowassa katika kijiji cha Ngarash wilayani Monduli mkoani Arusha.
Amesema hayati Lowassa amekuwa mtu wa kujituma kwa kufanyakazi kwa bidii na kwa weledi huku akiwa na msimamo katika kuyasimamia aliyoyaanzisha.
Amesema atamkumbuka kwa mambo matatu ambayo yamekuwa funzo kwa taifa ambayo ni ushupavu,ustahimilivu na ulezi.
“Haya mambo matatu yamekuwa funzo kwa taifa kwani aliyafanya bila kuyumba inabidi tuyaenzi kwa kufanyakazi kwa didii bila kusukumwa na wanaotuongoza”amesema.
Amesema ustahimilivu aliounyesha Lowassa katika nyanja zote hasa katika siasa na hii imepelekea hata uwepo wa 4R ambazo zinaendelea kufanyakazi ikiwemo maridhiano.
Sambamba na hayo amesema atakumbukwa kwa usimamizi wake wa miradi mikubwa ya maji ambayo imekuwa na manufaa makubwa kwa taifa.
“Kwa haya hapo somo tunalipata tukipewa dhamana za uongozi na kuaminika katika nafasi mbalimbali za serikali lazima tuwe na uthubutu na ubunifu pamoja na kusimamia na kutekeleza kwa weledi bila kuyumbishwa”Amesema.
Akizungumzia swala la ulezi amesema Lowassa amelea vijana wengi na kuwafundisha katika ngazi mbalimbali na hakuacha ulezi huo hata alipokuwa nje ya utumishi bado aliendelea kulea.
Amesema katika swala la elimu alihamasisha ujenzi wa shule za sekondari za kata ambapo serikali ilijenga shule hizo na mpaka sasa inaziendeleza ambapo kutoka shule 828 mwaka 2004 mpaka shule 4,578 mwaka 2023.
Sambamba na hayo ametoa rai kwa wanasiasa nchini kuendelea kufanya siasa za kistaarabu na kustahimiliana kwa kuweka maslahi ya nchi mbele.
Kwa upande wake waziri Mkuu ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya kuratibu mazishi Kassim Majaliwa amemshukuru Rais kwa usimamizi na ushari wake katika kuhakikisha hayati Edward Lowassa anazikwa kwa taratibu zote za kiserikali.
Kwa upande wake spika wa bunge Dkt. Tulia Akson ametoa rai kwa wananchi kuanza kujitafakari katika safari ya maisha wanatarajia kuacha alama gani ili pindi watakapoaga dunia waache funzo na alama kama alivyofanya Lowassa.
Wakizungumza kwa niaba ya familia watoto wa marehemu Lowassa ambae ni Richard Lowassa na Fredrick Lowassa wameshukuru wote waliojitokeza kuwafariji na kuwasaidia katika kipindi chote walichokuwa wanamuuguza baba yao mpaka umauti unamkuta
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mboye amesema historia ya Lowassa haitaweza kusahaulika ndani ya chama kwani ameweza kusaidia kupata ongezeko kubwa la wabunge wa upinzani bungeni na madiwani wengi wakati alipogombea urais katika chama hicho.