Na Sophia Kingimali
Aliekuwa Mkuu wa wilaya ya Monduli Gabriel Zakaria amesema jamii ya kimasai itaendelea kumkunbuka hayati Edward Ngoyai Lowassa kwa kuwaletea mabadiliko makubwa hasa katika sekta ya elimu.
Hayo ameyasema leo Februari 16,2024 katika kijiji cha Ngarash wilayani Monduli mkoa wa Arusha kwenye msiba wa aliyekuwa Waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa.
Amesema muamko mkubwa wa watoto wa kimasai kwenda shule uliletwa na uthubutu wake alioufanya kwa kupiga marufuku ngoma zilizokuwa zinachezwa na vijana kwani ndio zilikua zinachangia kwa kiasi kikubwa kwa vijana kukataa shule.
“Elimu kwa familia za kimasai ilikua changamoto sana na hii ilitokana na uwepo wa ngoma ya Esotho ambayo ilikua inachezwa na vijana mamoran vijana ambao wameenda jando hii ilikuwa inachezwa kipindi cha mavuno kwa hiyo vijana wa kike na wakiume wanajumuika katika kitu kikubwa alichokifanya marehem ni kupiga marufuku hiyo ngoma na leo tunashuhudia watoto wa kimasai wanaenda shule”amesema
Nae kiongozi wa kimila laigwanan Kipi Oshumo laizer amesema kwao ni pigo kubwa sana na wataendelea kumlilia na awatamsahau kwa mambo mengi ya maendeleo aliyowafanyia ikiwemo elimu na kuwajengea mabwawa makubwa ya maji kwa ajili ya mifugo yao.