Naibu Rasi Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Dkt. Coretha Komba akizungumza na wafanyakazi Chuo hicho wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wa namna ya kutumia mfumo mpya wa kielektroniki wa manunuzi ya Umma yaani National – e – Procurement System (NeST) yaliofanyika leo february 16, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Mkufunzi wa mafunzo ya namna ya kutumia mfumo mpya wa kielektroniki wa manunuzi ya Umma yaani National – e – Procurement System (NeST) Afisa Manunuzi Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe Bw. Jones Mapande akizungumza na wafanyakazi Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam wakiwa katika mafunzo ya namna ya kutumia mfumo mpya wa kielektroniki wa manunuzi ya Umma yaani National – e – Procurement System (NeST).
Naibu Rasi Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Dkt. Coretha Komba akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi Chuo hicho baada ya kumaliza mafunzo ya kutumia mfumo mpya wa kielektroniki wa manunuzi ya Umma yaani National – e – Procurement System (NeST).
………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam wamejengewa uwezo wa namna ya kutumia mfumo mpya wa kielektroniki wa manunuzi ya Umma yaani National – e – Procurement System (NeST) ambao umelenga kuleta ufanisi katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali.
Akizungumza leo FebruarI 16, 2024 Jijini Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku nne, Kaimu Naibu Rasi wa Ndaki ya Dar es Salaam Dkt. Coretha Komba, amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kutumia mfumo NeST kwa uweledi ambao unakuwa hali ya uwazi katika kuomba na kufanya manunuzi.
Dkt. Komba amesema kuwa kupitia mafunzo hayo, wafanyakazi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam watabadilika katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika kutumia mfumo wa NeST.
“Mafunzo yoyote ni muhimu kwa binadamu; ninaamini kwa mafunzo haya, tutabadilika katika kufanya manunuzi kupitia mfumo huu ambao ni rafiki katika utendaji wa kazi zetu”. Amebainisha Dkt. Komba.
Dkt. Komba amesisitiza umuhimu wa kutumia mfumo wa kielektroniki wa NeST kutokana unatoa fursa kwa mwombaji kujua maombi yake yamefikia hatua gani katika kufanya manunuzi.
Mkufunzi wa mafunzo hayo, Afisa Manunuzi Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe Bw. Jones Mapande, amesema kuwa wamekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo kwa watumishi wa Kitengo cha Manunuzi pamoja wa Idara ya Matumizi.
Bw. Mapande amesema kwa sasa matumizi yanapaswa kufanyika katika mfumo mpya wa NeST kama sheria ya manunuzi inavyoelekeza na kufata utaratibu wote. Hivyo, watumishi hawana budi kuwa na uelewa wa Mfumo huo.
“Mfumo huu mpya unaweka hali ya uwazi katika utekelezaji kuanzia Idara ya Matumizi, kuandaa mahitaji yake na kupeleka Kitengo cha Manunuzi kwa njia ya mfumo, na mununuzi haya yanafanyika kwa njia ya mfumo”. Anasisitiza Bw. Mapande.
Aidha, Bw. Mapande amefafanua kuwa mfumo wa NeST unatumika kwenye matumizi ya fedha jambo ambalo litasaidia kuwa na uwazi na kuokoa fedha nyingi za Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Nao baadhi ya Washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Afisa Manunuzi Bi. Renatha Mukinga pamoja na Mkutubi Bi. Reine Mdundo kutoka Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam, wamesema kuwa mafunzo hayo yanakwenda kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa manunuzi.