Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Nusrat Shaaban Hanje, aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali wa kuwajengea uwezo wa Kimamlaka Wakaguzi Wakuu wa Ndani ili kuzuia ubadhirifu na wizi wa mali za Umma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Fedha)
……..
Na. Peter Haule, WF, Dodoma
Serikali imesema kuwa imewaelekeza Maafisa Masuuli wote kuhakikisha wanawawezesha wakaguzi wa ndani kwa kuwapatia rasilimali fedha na nyenzo muhimu kulingana na mipango kazi ya vitengo iliyopitishwa na Kamati za Ukaguzi.
Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Nusrat Shaaban Hanje, aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali wa kuwajengea uwezo wa Kimamlaka Wakaguzi Wakuu wa Ndani ili kuzuia ubadhirifu na wizi wa mali za Umma
Mhe. Chande alisema kuwa Serikali kupitia Waraka Na. 02 wa Mwaka 2024 wa Katibu Mkuu Kiongozi kuhusu Uwajibikaji katika Kusimamia Rasilimali za Umma na Kushughulikia Hoja za Ukaguzi, umewaelekeza Maafisa Masuuli wote kutenga fedha za ukaguzi kwa kila mradi wa maendeleo ili kuwawezesha wakaguzi wa ndani kukagua kwa ufanisi na kudhibiti vihatarishi.
Alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha utendaji kazi wa wakaguzi wa ndani ikiwemo kufanya mapitio ya Sheria ya Fedha za Umma SURA 348, muundo wa Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali pamoja na vitengo vya ukaguzi wa ndani katika Wizara, Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi zote za Umma kwa lengo la kuongeza uhuru wa wakaguzi wa ndani katika kutekeleza majukumu yao.
Akijibu kuhusu wakaguzi wa ndani kuwakagua viongozi wao na kusababisha ufanisi mdogo, Mhe. Chande alisema kuwa Wakaguzi wa Ndani wa Serikali ni sehemu ya utekelezaji wa shughuli za Serikali za kila siku kwa kuwa wanakagua kabla mradi haujaanza, wakati inaendelea ili kupunguza au kuondoa kabisa changamoto zinazoweza kujitokeza.
Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ni taasisi nyingine ambayo inakagua kazi za Serikali baada ya kukamilika ili kuweza kubaini mapungufu yaliyopo na kuishauri Serikali.