Meneja Msaidizi Uchambuzi wa Sera ya fedha kutoka BoT John Rhodes Mero.
……………………
Na John Bukuku Zanzibar
Benki Kuu ya Tanzania imeeleza sababu iliyopelekea kuingia kwenye mfumo mpya wa sera ya fedha kuwa ni changamoto ambazo walizokutana nazo wakati wa utekelezaji wa mfumo wa zamani ambao ulipelekea ufanisi wa sera ya fedha kuanza kupungua kutokana na mabadiliko yaliyokuwa yanajitokeza kwenye kasi ya mzunguko wa fedha.
Hayo yamebainishwa Februari 15, 2024 na Meneja Msaidizi Uchambuzi wa Sera ya fedha kutoka BoT John Rhodes Mero wakati alipokuwa akizungumza na Fullshangwe Blog juu ya mfumo mpya wa sera ya fedha.
Amesema awali walikuwa wanatumia mfumo wa ujazo wa fedha ambapo walikuwa wanaangalia kiwango cha fedha ambacho kinaingia kwenye uchumi kiendane na mahitaji mbalimbali ya shughuli za uchumi.
“Kuanzia Januari tumeuanza kutumia mfumo wa riba ambao Sasa Benki kuu itakuwa inatangaza riba ya sera ya fedha na riba hii itakuwa inatoa mwelekeo wa sera ya fedha,pia ni riba ambayo itakuwa inatoa mwongozo wa riba zinazotozwa kwenye soko la fedha baina ya taasisi za kifedha kwa mikopo ya siku saba”, amesema Mero
Ameeleza kuwa mikopo inayochangia na mabenki kwenye soko la fedha itakuwa inaendana na riba ya Benki Kuu kwasababu wanategemea riba hiyo iwe inatembea kwenye wigo wa wastani wa asilimia mbili chini ya riba ya Benki kuu hadi asilimia mbili juu ya riba ya Benki kuu.
Riba hii ya Benki kuu inapatikana kwakutumia viashiria vya uchumi ambapo wataalam wanakaa wanafanya maoteo ya mfumuko wa bei,ukuaji wa uchumi na mwenendo wa uchumi kwa ujumla.
“Riba ambayo inapatikana baada ya kuangalia mwenendo umekaaje na kwa sasa kiashiria chetu cha kati Cha utekelezaji wa sera ya fedha hakitakuwa tena ni ujazo wa fedha bali kitakuwa ni maoteo ya mfumuko wa bei, ikioneka mfumuko wa bei unatarajiwa kuwa juu ya lengo letu Benki Kuu itapandisha riba ya sera ya fedha kuonesha tunaenda kubana kiwango cha ukwasi ambacho tunakiingiza kwenye uchumi”,
Amesema ikioneka mfumuko wa bei unatarajiwa kuwa chini ya lengo lao wanapunguza riba na hivyo kupelekea ujumbe rahisi kuwa taasisi za kifedha wataenda kukopa BoT na inakuwa ni rahisi kwao kwenda kutoa mikopo kwa riba nafuu.
Aidha, amesema riba ya Benki Kuu ni asilimia 5.5 na ni riba ya kwanza iliyoamuliwa kwa lengo la kuhakikisha wanapambana na mfumuko wa bei sanjari na kuchagiza shughuli za kijamii.
Mwisho ameeleza kuwa riba ya pili itatangazwa Aprili mwaka huu na hii ndiyo itatoa mwelekeo wa sera ya fedha na itakuwa unapeleka ujumbe ambao uko wazi ikilinganishwa na ya awali kwa sababu hii ya awali wadau wengi ambapo ni taasisi za fedha wakuwa kama wanajifunza namna ya kwenda na sera hiyo mpya ya fedha.