Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman atachuana na Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa , Juma Duni Haji ambaye anatetea kiti chake
Mheshimiwa Othman Masoud Othman amechukua fomu hiyo leo Februari 15, 2024 ili Kugombea Nafasi ya Mwenyekiti wa Chama hicho, Ngazi ya Taifa.
Mheshimiwa Othman amedhaminiwa na Wenyeviti na Makatibu wa ACT-Wazalendo katika Mikoa 27 ya Kichama, ya Tanzania Bara na Zanzibar ambapo imekabidhiwa leo katika hafla ambayo imeongozwa na Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Kigoma, Kiiza Mayeye iliyofanyika katika Ofisi kuu ya Chama hicho, Vuga Mjini Unguja.
Hadi sasa waliochukua fomu kugombea nafasi hiyo ni Mheshimiwa Othman Masoud Othman pamoja na Juma Duni Haji.
Othman Masoud anakabiliwa na kibarua kigumu kwa kukabiliana na Juma Duni Haji ambaye ni nguli wa siasa za upinzani visiwani Zanzibar na mwanzilishi wa chama cha Upinzani cha CUF kabla ya kuhamia chama cha ACT- Wazalendo na aliwahi kukaa rumande kwa miaka miwili na nusu misukosuko kadhaa ya kisiasa kwa kufungwa akituhumiwa kwa uhaini.
Juma Duni Haji ama ‘Babu Duni’ anavyojulikana kwa wafuasi wake, ni mwanasiasa mtiifu wa upinzani. Enzi za uhai wa Seif Sharif Hamad (almaarufu Maalim Seif) hadi anafariki, hakukushuhudiwa mvutano wa hadharani kati ya Babu Duni na Maalim.
Yuko kwenye siasa za upinzani kwa takribani miongo mitatu sasa. Ameshika nafasi mbalimbali za ndani ya Chama cha Wananchi (CUF); Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha Taifa, Makamu Mwenyekiti, na Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa.