Meneja Msaidizi Idara ya Utafiti Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dkt. Lusajo Mwankemwa akizungumza katika semina ya waandishi wa habari na wahariri kuhusu majukumu ya Benki kuu ya Tanzania (BoT) inayofanyika Ofisi za Makao Makuu Ndogo Zanzibar kuanzia Februari 14-16, 2024.
Meneja Msaidizi Idara ya Utafiti Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dkt. Lusajo Mwankemwa akifafanua jambo wakati akizungumza katika semina ya waandishi wa habari na wahariri kuhusu majukumu ya Benki kuu ya Tanzania (BoT) inayofanyika Ofisi za Makao Makuu Ndogo Zanzibar kuanzia Februari 14-16, 2024. kulia ni Sheha Haji Sheha Afisa Habari Maelezo Zanzibar na kushoto ni John Rhodes Mero Meneja Msaidizi Uchambuzi wa Sera ya Fedha BoT.
……………………………..
NA JOHN BUKUKU, ZANZIBAR
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewajengea uwezo wahariri na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini kuhusu utekelezaji wa majukumu yao pamoja na mabadiliko ya utekelezaji wa sera ya fedha ambayo imeanza kufanya kazi januari 19, 2024 jambo ambalo litasaidia kutekeleza majukumu yao kwa weledi.
Akizungumza katika semina ya wahariri na wanahabari kuhusu majukumu ya Benki kuu ya Tanzania (BoT) inayofanyika Ofisi za Makao Makuu Ndogo Zanzibar kuanzia Februari 14-16, 2024, Meneja Msaidizi Idara ya Utafiti Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dkt. Lusajo Mwankemwa, amesema kuwa elimu hiyo inakwenda kuwasaidia waandishi wa habari kujua mabadiliko ya utekelezaji wa sera ya fedha ambayo imeanza kutekelezwa hivi karibuni.
Dkt. Mwankemwa amesema kuwa wameona vizuri waandishi wa habari na wahariri kujua majukumu ya BoT kulingana na sheria ya Benki Kuu ya mwaka 1966 pamoja na mabadiliko yake ya mwaka 2006 ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Amesema kuwa Benki Kuu inajukumu mbalimbali ikiwemo uandaaji na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei.
“BoT ina jukumu la uandaaji na usambazaji wa sarafu ambayo inatumika, kusimamia mabenki ya biashara na kutoa leseni pamoja na kusimamia mifumo ya malipo hapa nchini” amesema Dkt. Mwankemwa.
Dkt. Mwankemwa amesema BoT inatoa huduma ya kibenki kwa serikali ya Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na kutoa ushauri wa kifedha ili kufikia malengo tarajiwa.
Amefafanua kuwa miongoni mwa majukumu yao mengine ni kusimamia sekta ya fedha nchini, pamoja na kutoa mikopo kwa benki za biashara. Aidha Benki Kuu kwa niaba ya Serikali, inashirikiana na taasisi mbalimbali za kimataifa kwa lengo la kuimarisha mahusiano baina ya Serikali ya Tanzania na taasisi za kimataifa, ikiwemo Shirika la Fedha Duniani, IMF na Benki ya Dunia, WB.
Meneja Mawasiliano Benki Kuu ya Tanzania(BoT) Bi. Vick Msina akifafanua mambo kadhaa kwa wahariri wa vyombo vya habari na waandishi wa habari katika semina kuhusu majukumu ya Benki kuu ya Tanzania (BoT) inayofanyika Ofisi za Makao Makuu Ndogo Zanzibar kuanzia Februari 14-16, 2024. kulia ni Sheha Haji Sheha Afisa Habari Maelezo Zanzibar.
Picha zikionesha waandishi wa habari na wahariri mbalimbali wakiwa katika semina hiyo inayofanyika kwa siku tatu kwenye Ofisi za Makao Makuu Ndogo Zanzibar kuanzia Februari 14-16, 2024. kulia ni Sheha Haji Sheha Afisa Habari Maelezo Zanzibar.