Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera kufungua Mkutano wa wadau wa afya wanaohudumiwa na MSD katika Kanda ya Mbeya.
……..
Na Joachim Nyambo, Mbeya
WADAU wa Bohari ya Dawa(MSD) kupitia Wizara ya Afya wametakiwa kufanya maoteo ya bidhaa za afya kwa usahihi na kwa wakati ili kuiwezesha taasisi hiyo kuwa na takwimu katika kuagiza kutoka kwa wazazlishaji na wasghitiri hivyo kuboresha upatikanaji wa bidhaa hizo.
Kadhalika wamehimizwa kusimamia matumizi sahihi ya takwimu za mnyororo wa ugavui ili ziwasaidie kufanya maamuzi sahihi juu ya bidhaa za afya katika maeneo yao.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa alihimiza hayo alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Juma Homera kufungua Mkutano wa wadau wa afya wanaohudumiwa na MSD katika Kanda ya Mbeya.
MSD Kanda ya Mbeya inahudumia mikoa ya Mbeya, Songwe, na Rukwa pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Makete iliyopo mkoani Njombe.
Malisa aliwasihi waganga wakuu wa wilaya na wafamasia wa mikoa kukagua na kufuatilia matumizi ya bidhaa za afya katika kila ngazi ili kudhibiti mianya ya upotevu wa bidhaa hizo.
Aliwataka pia wadau wa Bohari kutambuwa kuwa wanalo jukumu kubwa la kuvisimamia vituo vya kutolea huduma za afya katika maeneo yao ili viweze kukusanya mapato ya kutosha yanayotokana na uchangiaji wa huduma za afya ili viweze kununua bidhaa zinazohitajika sambamba na kusimamia mnyororo wa ugavi wa bidhaa hizo.
“Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuongeza fedha inayotengwa kwaajili ya bajeti ya kununulia bidhaa za afya ili kuboresha utoaji wa huduma za afya. Kila mmoja hapa ana jukumu la kusimamia matumizi sahihi ya bidhaa za afya ili kuleta tija kwa wananchi.” Alisisitiza Maliza.
“Tukasimamie ukusanyaji wa mapato katika vituo vyetu vya kutolea huduma za Afya ili pia vituo viweze kulipa madeni yaliyopo MSD kwa wakati mara baada ya kupokea shehena ya bidhaa na kurepusha madeni yasiyo ya lazima.”
Mkuu huyo wa wilaya alisema kwa kutekeleza hayo wananchi watapata huduma bora zaidi kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya bila manung’uniko.
Awali Meneja wa MSD Kanda ya Mbeya, Marco Masala alisema lengo la mkutano ilikuwa ni wadau kupata fursa ya kujadiliana na kutatua changamoto za upatikanaji wa wa bidhaa za afya katika mikoa yao ili watendaji waweze kutimiza wajibu wao ipasavyo.