Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Idara ya Uchumi, Profesa Aurelia Kamuzora.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Sarikali imetakiwa kupeleka huduma ya mtandao katika vijiji ambavyo hakuna mawasiliano ili waweze kupata utabiri na kunufaika na taarifa za hali ya hewa ambazo kwa sasa zimekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa kupitia shughuli za kilimo.
Imebainika taarifa za utabiri wa hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zimekuwa na usahihi na kuaminiwa jambo ambalo wakulima ambao asilimia kubwa wanaishi vijijini wamekuwa wakizitumia katika kuandaa mashamba pamoja na kupanda mazao kulinga na mazingira ya taarifa za utabiri wa hali ya hewa.
Akizungumza na mwandishi wetu Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Profesa Aurelia Kamuzora, amesema kuwa uwepo mvua kubwa ni fursa kwa watanzania katika kufanya shughuli za kilimo kwani ni sekta ambayo inachangia kutoa ajira kwa asilimia 64.
Profesa Kamuzora amesema kuwa kiuchumi mvua zinaleta fedha za kigeni kupitia kilimo cha kimkakati ikiwemo kahawa, pamba pamoja na korosho ambapo mazao yake hayahitaji umwagiliaji.
“Baadhi ya vijiji hakuna mawasiliano kutokana na tatizo la mtandao, TMA wanafanya kazi nzuri na ili tuweze kufaidi wote utabiri wa hali ya hewa; Serikali itusaidia kupeleka mtandao maeneo ambayo hakuna kwa sababu watumiaji wa kubwa wa utabiri wa hali ya hewa ni wakulima ambao wanaishi vijijini” amesema Profesa Kamuzora.
Profesa Kamuzora ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Idara ya Uchumi, amesema kuwa TMA waliposema mwaka huu mvua zitanyesha kubwa wakulima walianza kuchangamkia fursa kwa kuandaa mashamba na baada ya kunyesha walipanda mazao.
Uchumi huyo amesisitiza umuhimu wa usahihi wa utabiri wa hali ya hewa kwa wakulima katika utekelezaji wa kazi zao, huku akiwataka wananchi katika kipindi hiki cha mvua kubwa kutengeneza miundombinu ya kuvuna maji ambayo yanaweza kuwa msaada katika kipindi cha ukame.
“Mvua zina faida kubwa katika uchumi kuliko hasara ambazo tumeziona ikiwemo uharibifu wa miundombinu; mfano zao la kahawa limeshika nafasi ya pili mwaka 2023 kwa kuchangia upatikanaji wa fedha za kigeni, na mwaka ujao tunatarajia kupata fedha zaidi kutokana na mvua kubwa ambazo zitachangia upatikanaji zao la kahawa ” amesema Profesa Kamuzora.
Ameeleza kuwa kwa sasa vijiji vingi wamelima zao la kahawa kutokana na uwepo wa mvua za kutosha, hivyo mwaka 2025 wanatarajia kupata tani nyingi tofauti na mwaka 2023 ambapo walipata tani 80,000.
Profesa Kamuzora amesema kuwa teknolojia ya kilimo nchini bado inategemea mvua ili wakulima waweze kupata mazao ya kutosha, huku akieleza kuwa uwepo wa mvua ni neema katika utekelezaji wa shughuli za uchumi kupitia kilimo tofauti na baadhi ya watu wachache wanaotafsiri kama hasara hasa wanaoishi mjini.
“Miaka michache iliyopitia tulishuudia ukame katika maeneo mengi, tuliona mazao yakikauka, mifugo ikafa ilikuwa ni janga kubwa, lakini sasa mvua imeleta malisho ya mifugo na mazao yamestawi vizuri” amesema Profesa Kamuzora.
Profesa Kamuzora amesema kuwa mwaka 2024 wakulima wanatarajia kupata mazao ya kutosha jambo ambalo litasaidia kupunguza mfumuko wa bei sokoni pamoja na kupata fursa ya kuuza mazao nje ya nchi na kupata fedha za kigeni ambazo zitachangia kukua kwa pato la Taifa.
Usahihi wa utabiri wa hali ya hewa unaopatikana kwa sasa kutoka TMA unatokana na vifaa madhubuti ambavyo vimewekwa na serikali katika kipindi cha awamu ya sita.
Uboreshaji huo umejikita katika kuboresha miundombinu ya hali ya hewa ikiwemo ununuzi wa mitambo na vifaa vya kisasa vya uangazi wa hali ya hewa, ununuzi wa Rada za hali ya hewa; utekelezaji wa mfumo wa kudhibiti ubora wa huduma pamoja na kujenga uwezo kwa watumishi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka TMA serikali ilitenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 50 katika bajeti ya maendeleo kwa ajili ya ununuzi wa Rada za hali ya hewa, kununua vifaa vya hali ya hewa, ukarabati wa vituo vya hali ya hewa pamoja na ujenzi wa Kituo cha Hali ya Hewa cha Kanda ya Mashariki ili kuongeza ufanisi.
Mafanikio haya yameifanya TMA kuweza kutimiza majukumu yake ya utoaji wa huduma, uratibu na udhibiti wa shughuli za hali ya hewa nchini kama ilivyoelekezwa katika Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019
TMA inatoa wito kwa wananchi kuendelea kufuatilia na kutumia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa kwa ajili ya shughuli za kijamii na kiuchumi kwa maendeleo ya Taifa.