Nyumba ya jumuiya ya watumia maji(CBWSO)inayondelea kujengwa ka ajili ya mradi wa maji Misechela-Liwanga unaotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilayani Tunduru kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni 3.Na Mwandishi wetu, Tunduru
BAADHI ya wakazi wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wameipongeza serikali kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kwa kutimiza ahadi ya kuwapatia huduma ya maji safi.
Walisema, kwa muda mrefu baadhi ya vijiji vya wilaya ya Tunduru vilikabiliwa na changamoto kubwa ya huduma ya maji safi na salama,hivyo kulazimika wananchi kutumia maji ya visima vya asili na mito ambayo hayakuwa safi na salama kwa matumizi ya binadamu.
Issa Athuman mkazi wa kijiji cha Chiwana wilayani humo alisema,kufikishwa kwa mtandao wa maji ya bomba katika kijiji chao imesaidia sana kumaliza changamoto hiyo iliyowatesa kwa muda mrefu na ambayo ilikwamisha kushindwa kushiriki kazi za kujitolea na zile za kujiletea maendeleo yao.
Jemshina Hamis alisema,wanawake wa kijiji hicho ndiyo walikuwa waathirika wakubwa kwa kuwa walikuwa wanaamka usiku wa manane kwenda kusaka maji kwa ajili ya familia zao huku wakiwaacha waume zao kitandani,hali hiyo iliwakosesha furaha na amani katika maisha yao.
Hadija Chigweje mkazi wa mtaa wa kijiji cha Tuwemacho alisema, baadhi ya wanawake wenzao ndo zao zimevunjika kwa sababu ya kuchelewa kurudi nyumbani wanapokwenda kutafuta maji kwenye mito na mabonde ambayo yanayopatikana mbali na makazi yao.Kwa upande wake meneja wa Ruwasa wilaya ya Tunduru Mhandisi Maua Mgallah alieleza kuwa, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 wamepanga kutumiza zaidi ya Sh.bilioni 5,473,744,522.32 kwa ajili ya kutekeleza miradi 6 mipya ya maji.
Mgallah alitaja baadhi ya miradi hiyo ambayo imeanza kutekelezwa ni mradi wa maji Tuwemacho utakaogharimu Sh.bilioni 1,054,232,603.55 na mradi wa maji Msinji unaotekelezwa kwa Sh.bilioni 1,069,014,450.00.
Miradi mingine ni Hulia unaotekelezwa kwa Sh.bilioni 1,206,605,519.28,mradi wa maji Namwinyu wenye thamani ya Sh.milioni 450,000,000 na mradi wa maji Nakapanya ambao umetengewa jumla ya Sh.milioni 150,000,000.00.
Mgallah alisema,miradi hiyo ipo hatua mbalimbali za utekelezaji wake na itakapokamilika itaongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa asilimia 7.2 hivyo kufikisha asilimia 89.8 katika maeneo ya vijijini.
Aidha alisema,kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Ruwasa wilaya ya Tunduru ilitengewa Sh.bilioni 3,890,260,834.14 ambazo zilitumika kutekeleza jumla ya miradi mitano pamoja na uchimbaji wa visima.
Kwa mujibu wa Mgallah miradi ni Masuguru (2,416,574,071.52) utakaonufaisha vijiji saba,mradi wa Ligoma-Makoteni-Chalinze-Majimaji na Imani (1,442,936,167.98) ambao unatekelezwa kwenye vijiji vitano.
Pia miradi mingine ni Muhuwesi( milioni 175,000,000.00)mradi wa maji Semeni(milioni 175,000,000.00 uchimbaji wa visima katika vijiji 18(Sh.milioni 514,220,272.56) na mradi wa maji Ndeja-Mbesa awamu ya pili unaotekelezwa kwa gharama ya Sh.bilioni 1,500,000,000.
Mgallah alieleza kuwa,miradi hiyo imewezesha kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya hiyo kwa asilimia 12.6 ambapo zaidi ya watu 43,625 wamenufaika.
Alisema,katika wilaya ya Tundru vijiji vinavyo hudumiwa na Ruwasa ni 139 kati ya hivyo 116 vimefikiwa na huduma ya maji na vijiji 58 vina miundombinu ya mtandao wa bomba.
Hata hivyo alieleza kuwa, vijiji 58 vina miundombinu ya maji ya kupampu kwa mkono na vijiji 23 havina kabisa huduma ya maji safi na salama huku upatikanaji wa huduma ya hiyo ni wastani wa asilimia 70.06 huku idadi ya watu wanaopata maji safi na salama ni 235,680 kati ya watu 336,380.
Alisema,lengo la Ruwasa ni kufikisha asilimia 85 ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wote waishio maeneo ya vijijini ifikapo mwaka 2025.
Mgallah alieleza kuwa,kabla ya Ruwasa upatikanaji wa maji katika wilaya ya Tunduru ulikuwa asilimia 49.89 lakini baada ya kuanzishwa kwa Ruwasa mwaka 2019 upatikanaji wa huduma yam aji vijijini imeongezeka hadi kufikia asilimia 70.06.