Baadhi ya wanafunzi wakishiriki kupanda miti kuzunguka mlima wa Wamweru katika Kijiji cha Mirumba halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi.
……..
Na. Zillipa Joseph, KATAVI
Wakazi wa Mirumba katika Halmashauri ya MPIMBWE wilaya ya Mlele mkoani Katavi wameanza kupanda miti kuzunguka mlima wa WAMWERU ili kuweza kurudisha uoto wa asili katika msitu wa kimila wa watu wa kabila la Wamweru.
Msitu huo ambao pia ni chanzo kikubwa cha maji ulianza kupoteza uasilia wake kutokana na uvamizi wa baadhi ya watu kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu.
Akizungungumza na mwandishi wa habari hizi Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Watu, Simba, na Mazingira (WASIMA) Jonathan Viega amesema katika Kijiji cha Mirumba Wana mpango wa kupanda miti elfu arobaini na sita.
Bwana Viega amefafanua kuwa licha ya miti hiyo kupandwa eneo la msitu wa mlima pia kila kaya itaruhusiwa kuchukua miche zaidi ya kumi na kupanda katika kaya zao.
Aliongeza kuwa miti hiyo ikikua itasaidia kupata nishati ya kuni kwa kaya na kupunguza kukata miti iliyohifadhiwa.
Aidha aliongeza kuwa kwa Halmashauri ya Mpimbwe wamepanga kupanda jumla ya miti elfu themanini na sita kwa msimu huu wa bajeti.
Kwa upande wake Afisa Mazingira wa halmashauri hiyo Mwalu Saka amewaonya watu juu ya tabia ya uharibifu wa Mazingira.
Bi Josephine Rupia ni Afisa Wanyama Pori Mkuu katika mkoa wa Katavi, alisema ipo haja ya kifundisha watoto wetu umuhimu wa Mazingira ili hata wanapokuwa watu wataweza kuyathamini Mazingira.
Alisema Mazingira ni muhimu kwa binadamu na viumbe wengine.
‘Hivi mnavyoona mkoa wetu unapata mvua za kutosha ni kutokana na kuwa karibu na hifadhi ya Taifa ya Katavi ambayo ina miti ya kutosha’ alisema.
Bi. Rupia aliongeza kuwa ukataji wa miti hovyo unasanabisha kukosekana kwa mvua.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliojitokeza kupanda miti, walilishukuru shirika la WASIMA kwa kuwapatia miti bure kwa ajili ya kupanda katika kaya zao.