Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akitoa salamu za pole kwa familia, viongozi na wananchi kwa ujumla wakati wa kuaga mwili wa Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam tarehe 13 Februari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwafariji wanafamilia wa Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa mara baada ya kutoa heshima za mwisho kwa hayati Edward Lowassa katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam tarehe 13 Februari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akitoa heshima za mwisho kwa Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam tarehe 13 Februari 2024.
…………………….
Na Sophia Kingimali.
Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema serikali itaendelea kuthamini mchango mkubwa alioutoa Hayati Edward Ngoyai Lowassa katika maendeleo ya nchi katika kipindi chote cha uhai wake na utumishi wake.
Hayo ameyasema leo Februari 13,2024 wakati akiongoza viongozi na wakazi wa Dar es salaam kutoa heshima zao za mwisho katika viwanja vya karimjee jijini jijini hapo.
Amesema lowasa alijitolea vyema katika maendeleo ya Taifa kwa kutumia vipawa na karama zake katika kuleta maendeleo na kuwatumikia wananchi katika nyazifa mbalimbali alizowahi kushika.
“Ni vizuri kila mtu ajikumbushe wajibu alionao kwa taifa hii itatufanya kuyakumbuka na kuyaenzi kwa vitendo mazuri yote yanayotokana na maisha ya hayati Lowassa”Amesema.
Aidha Dkt Mpango ametoa rai kwa wananchi hasa vijana kumuenzi hayati Lowassa kwa kutumia fursa mbalimbali kujipatia elimu kwani alikuwa kinara katika elimu na aliipigania kwa vitendo.
Ameaema Lowassa aliweza kuisimamia elimu kwa vitendo kwa kuandaa sera na mikakati mbalimbali ya elimu ikiwemo ujenzi wa shule za kata.
“Haya pamoja ya kuwa mzalendo katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu,mazingira lakini pia alikua mcha Mungu hivyo ni vyema tukafuata hatua zake ili tumuenzi kwa vitendo”Amesema Dkt Mpango.
Kwa upande wake,RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema namna bora ya kumuenzi Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa ni kuendelea kuyaishi maono yake ya uzalendo, uwajibikaji ili iwe dira ya kuzidi kujenga umoja na kupiga hatua za maendeleo nchini.
Nimejifunza mengi kutoka kwa Hayati Edward Ngoyai Lowassa ukiwemo uzalendo, uwajibikaji, ushirikiano na watu wa makundi yote na kuweka mbele maslahi ya nchi”Amesema Rais Dkt Mwinyi.
Nae,Jaji mkuu mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba amesema pamoja na changamoto alizonazo Hayati Lowassa lakini ameacha funzo kubwa kwa viongozi kwa moyo wake uvumilivu.
Kwa upande wake Waziri mkuu mstaafu Fredrick Sumaye amewataka viongozi kuhakikisha wanaacha alama katika taifa kama alivyofanya hayati Lowassa kwani maisha yake yote yalikuwa ya kujituma kwa kuwatumikia wananchi katika nyanja zote ikiwemo kisiasa na kijamii.
Akizungumza kwa niaba ya familia mtoto wa marehemu ambae pia ni mbunge wa Monduli Fredy Lowassa ameishukuru Serikali hasa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa karibu na familia tangu baba yao alipougua mpaka umauti ulipomkuta.