Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Bw. Abdillah Mataka katika Wizara ya Mambo ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki akichangia hoja kwenye Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati wa EAC uliokuwa ukiendelea katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha.
Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Nishati Bw. Petro Lyatuu akiongoza Mkutano wa 16 Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati uliokuwa ukiendelea katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mkutano wa 16 Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati uliokuwa ukiendelea katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha
Mkutano wa 16 Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati ukiendelea katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha
……………………
Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umenza leo tarehe 12 Februari 2024 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha.
Mkutano huo wa siku tatu kuanzia February 12 hadi 14, 2024 utafanyika katika ngazi tatu; ngazi ya Wataalamu tarehe 12 Februari 2024, ngazi ya Makatibu Wakuu tarehe 13 Februari 2024 na kuhitimishwa katika ngazi ya Mawaziri tarehe 14 Februari 2024.
Mkutano huo unatarajiwa kupokea na kujadili taarifa mbalimbali za maendeleo ya sekta ya nishati katika Jumuiya. Vilevile kuweka mikakati ya pamoja ya kutatua chagamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika na endelevu katika Jumuiya.
Maeneo ya sekta ya nishati yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni; umeme, mafuta na nishati jadidifu.
Awali akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa ngazi ya wataalamu Mwenyekiti wa Mkutano huo Bw. Petro Lyatuu, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Nishati – Tanzania ameeleza kuwa licha ya mafanikio yaliyofikiwa katika sekta hiyo bado mchango na weledi wa wataalamu hao unahitajika ili kutatua changamoto zilizopo na hatimaye kufikia malengo yanayotarajiwa na Jumuiya.
Bwana Latyuu ametoa rai kwa watalam hao kujikita katika kujadili na kuyapatia ufumbuzi wa kudumu masuala muhimu yatakayojili katika mkutano huo kwa manufaa ya Jumuiya.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo wa ngazi ya wataalamu unaongozwa na Bw. Abdillah Mataka Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mkutano huo unatarajiwa hutimishwa tarehe 14 Februari 2024 katika ngazi ya Mawaziri wanaosimamia sekta ya nishati umehudhiriwa na wajumbe kutoka Nchi zote saba (7) wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.