Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Angelina Adam Malembeka, bungeni jijini Dodoma, aliyetaka kufahamu wakati ambapo Serikali itabadili mwonekano wa noti na sarafu ili kutoa fursa ya kuweka picha ya Rais Mwanamke wa kwanza Tanzania. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Fedha)
……….
Na. Peter Haule, WF, Dodoma
Serikali imesema kuwa miongoni mwa sababu ya kuondoa picha za viongozi kwenye sarafu ya Tanzania ilikuwa ni gharama za mara kwa mara za uchapishaji wa noti kwa ajili ya kubadilisha picha za viongozi baada ya muda wao wa kuwa madarakani kukoma.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge Viti Maalum, Mhe. Angelina Adam Malembeka, aliyetaka kufahamu wakati ambao Serikali itabadili mwonekano wa noti na sarafu ili kutoa fursa ya kuweka picha ya Rais Mwanamke wa kwanza Tanzania.
Mhe. Chande alisema kuwa uamuzi wa kuondoa picha ya Rais kwenye noti ulifanyika katika kipindi cha Awamu ya Tatu chini ya Rais mstaafu Hayati Benjamin William Mkapa, kuanzia toleo la noti la mwaka 1997 ambapo picha ya Kiongozi wa nchi iliondolewa.
Alisema kuwa picha hiyo iliondolewa na badala yake ikawekwa picha za wanyama kama vile Tembo kwenye noti ya shilingi 10,000, Kifaru kwenye noti ya shilingi 5,000 na Simba kwenye noti ya shilingi 2,000 ili kuondoa gharama za mara kwa mara za uchapishaji wa noti.
Aidha, alisema kuwa katika kuenzi michango ya waasisi wa Taifa la Tanzania, noti ya shilingi 1,000 imeendelea kuchapishwa ikiwa na picha ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na noti ya shilingi 500 ilichapichwa ikiwa na picha ya Rais wa awamu ya kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.
Hata hivyo aliongeza kuwa, noti ya shilingi 500 ilibadilishwa kuwa sarafu mwaka 2014 ambapo picha ya Hayati Sheikh Abeid Amani Karume imeendelea kuwepo.