Daraja kubwa la Mto Muhuwesi lililopo Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma limefunikwa na maji kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha.
Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mheshimiwa Julius Mtatiro ambaye ameamua daraja hilo lifungwe kwa muda ili kuepusha madhara
……….
Na Albano Midelo,Tunduru
Daraja kubwa la Mto Muhuwesi lililopo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma limejaa maji hadi juu na kutishia usalama wa watu na mali.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mheshimiwa Julius Mtatiro amesema kujaa kwa katika mto Muhuwesi kumetokana mvua kubwa zinazonyesha ukanda wa Morogoro na Selous.
“Kwa hiyo tumechukua uamuzi wa haraka wa kufunga barabara kuu ya Mangaka – Tunduru Mjini kwa muda. Eneo la barabara linalofungwa ni eneo la mto lililo kati ya kata za Muhuwesi na Majimaji”,amesema Mtatiro.
Amebainisha kuwa Magari yanayotokea Mbeya, Iringa, Songea na Mkoa wote wa Ruvuma kuelekea Mkoa wa Lindi, Mtwara, Pwani na Dar yatakapofika Tunduru Mjini yapaki na kupumzika kusubiri hali iwe sawa kwenye Mto Muhuwesi.
Amesema magari yanayotokea mikoa ya Lindi , Mtwara, Pwani na Dar Es Salaam kwenda Tunduru, yanashauriwa kusimama na kupaki Nakapanya, Namiungo au Majimaji
Ametahadharisha kuwa madereva wasilazimishe kuvuka katika daraja hilo kwa sababu wanaweza kuleta madhara kwa watu na mali.