Angela Msimbira OR-TAMISEMI
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeishauri Serikali kuona umuhimu wa kuipelekea fedha za kutosha TARURA kwa kadiri ya bajeti ilivyoainishwa ili iweze kukabiliana na hali mbaya ya miundombinu nchini.
Ushauri huo umetolewa Bungeni leo Februari 13, 2024 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mbunge wa Mikumi Mheshimiwa Dennis Londo wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kipindi cha kuanzia Februari, 2023 hadi Januari, 2024
Amesema kamati haijaridhishwa na hali ya upelekaji wa fedha za bajeti kwa TARURA, ikizingatiwa kuwa katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwepo uharibifu wa miundombinu ya barabara nchini uliotokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika sehemu kubwa ya nchi.
“Ikumbukwe kuwa Serikali iliahidi ndani ya Bunge lako kuwa pamoja na bajeti ya Bilioni 808.02 Serikali ingetoa Bilioni 350 za ziada kwa TARURA. Kamati inasikitika kwamba, hata fedha hizi pia hazijapokelewa, hivyo tunaiomba Serikali iweze kutoa fedha kwa wakati ili kutatua changamoto za miundombinu nchini “ amesisitiza Mheshimiwa Londo.
Aidha, amesema Kamati imeiomba Serikali kuhakikisha inaiongezea bajeti TARURA kufikia shilingi trilioni 1.64 kutoka shilingi bilioni 710 kwa miaka minne mfululizo ili kufikia malengo ya asilimia 70 ya barabara kuwa za changarawe, asilimia 3 kuwa barabara za lami.
Pia, imeitaka Serikali kuhakikisha inasimamia kwa umakini taratibu za manunuzi kulingana na uwezo wa wakandarasi wanaoomba kazi na utekelezaji wa miradi husika.
Vilevile, wameielekeza Serikali kutekeleza mchakato wa kuanzisha Hati Fungani (TARURA SAMIA INFRASTRUCTURE BOND) kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara pamoja na kutafuta vyanzo vya fedha mbadala ikiwemo kushirikisha sekta binafsi ili kuiwezesha TARURA kuwa na fedha za uhakika za kutekeleza miradi ya barabara.