Diwani wa Mahina (CCM) Alphonce Francis kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi,akifungua mafunzo ya wajumbe wa serikali za mitaa na wasimamizi wa mradi wa kupunguza umasikini (TPRP) wa mitaa ya Igelegele na Kagomu,leo.
Wajumbe wa serikali za mitaa na wasimamizi wa mradi wa Jengo la Upasuaji kutoka mitaa ya Kagomu na Igelegele,Kata ya Mahina wakimsikiliza Diwani wa kata hiyo,Alphonce Francis (CCM) wakati wa mafunzo aliyoyafungua leo.
Mhasibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Jiji la Mwanza,Zawadi Hussein,leo akitoa mada ya ya taratibu za uhasibu kwa wasimamizi wa mradi wa jengo la upasuaji na wajumbe wa serikali za mitaa ya Kagomu na Igelegele.
Wajumbe na wasimamizi wa mradi wa jengo la upasuaji katika zahanati ya Mahina,leo wakifuatilia mada kutoka kwa Mhasibu wa TASAF Jiji, Zawadi Hussein (mbele kuli) wakati wa mafunzo yaliyofanyika Mahina Sekondari.
Ofisa Ufuatiliaji wa Miradi ya TASAF Jiji la Mwanza,James Hitler, leo akiwafundisha wajumbe wa serikali ya mtaa na wasimamizi wa mradi,namna ya kufuatilia na kusimamia miradi. (Picha zote na Baltazar Mashaka)
……….
NA BALTAZAR MASHAKA, NYAMAGANA
DIWANI wa Mahina (CCM),Alphonce Francis amesema mradi wa Jengo la Upasuaji la Zahanati ya Mahina unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa zaidi ya sh. milioni 123 utatatua changamoto ya huduma hiyo kwa wananchi wa kata hiyo.
Francis amesema hayo niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Amina Makilagi,leo wakati akifungua mafunzo kwa Wajumbe wa Serikali ya Mtaa na Kamati ya Usimamizi wa mradi wa huo kutoka mitaa ya Kagomu na Igelegele.
Amesema mradi huo unaotekelezwa katika Zahanati ya Mahina utakapokamilika utaondoa changamoto ya tiba ya upasuaji kwa wakazi wa Kata ya Mahina, na kuipongeza serikali kwa kuboresha huduma za afya ikiwemo kujenga miundombinu, kununua dawa,vifaa tiba na vitendanishi na hivyo wananchi waiunge mkono.
“Tumwombee Mh.Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kuwaletea Watanzania maendeleo pamoja na kuboresha huduma za afya zikiwemo za wajawazito na hakuna mwanamke atapoteza maisha akijifungua,tunawashukuru wadau wanaoishika mkono serikali na kuiwezesha kuhudumia wananchi wake,” amesema Francis.
Ameeleza mradi wa jengo la upasuaji unaokwenda sambamba na mradi wa OPD ambao umefikia asilimia 80,utaiwezesha zahamati ya Mahina kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya chenye vifaa vya kisasa itakapokamilika na hivyo jamii ishiriki kuchangia asilimia 10 ya nguvu kazi yao sawa na milioni 8 mradi huo ukamilike na kuwapa manufaa.
“Mnataka viongozi mliowachagua wawaletee nini, tushiriki na kuiunga mkono serikali inayogharamia asilimia 90 ya mradi na jamii asilimia 10 na mfurahi kupata mradi wenye thamani ya zaidi ya sh.milioni 123, msiwe sehemu ya hujuma ya mradi huu ambao ni mali yenu na tuufanye tuandike historia,”amesema Francis.
Diwani huyo wa Mahina amesema,hatakuwa radhi na hatakubali kuona mradi huo unakwama au unaondolewa sababu ya usimamizi na kusistiza kuwa ni lazima watu wachache waumie kwa manufaa ya wengine na vizazi vijavyo ikizingatiwa miradi wanayoitumia watu waliwajibika kuifanya wakaacha alama.
Katibu wa CCM Kata ya Mahina,Vitalis Makorosho amewataka wasimamizi wa mradi huo wa kimkakati kujitoa kuusimamia kwa weledi ulete manufaa na kuonesha imani kwa jamii iliyowachagua kuusimamia.
“Maendeleo hayaji bila kujitoa,tukijitoa na kuukamilisha thamani ya fedha ikaonekana hata waliotuletea mradi huo wa jingo la upasuaji watafarijika,”amesema na kuongeza kuwa katika usimamizi wa maslahi ya watu halazi damu na hana mzaha.
Naye mkazi wa Igelegele na mmoja wasimamizi wa mradi huo wa jengo la upasuaji,Zihaya Khalid, ameahidi kutumia elimu na alichojifunza kuwaelimisha wananchi au jamii faida na manufaa ya mradi hasa akinamama ambao ni wanufaika wakubwa wanapopata changamoto ya kujifungua kwa njia ya kawaida.
“Sisi akinamama lazima tujivune kupata mradi huu sababu utakuwa na manufaa kwetu kuliko watu wengine,hivyo nitawajibika kuwaelimisha wanaodhani mradi hauna maslahi kwao na kuwahamasisha kujitolea ili ukamilike,”amesema.
Kwa upande wake Mratibu wa TASAF Jiji la Mwanza, Peter Ngagani ameeleza kuwa serikali imewekeza sh.milioni 123.7 katika mradi huo wa afya na mfuko umejipanga kufanya mikutano ya kuhamasisha jamii inayonufaika kuchangia nguvu kazi yao ama fedha.