Diwani wa Mahina (CCM) Alphonce Francis wa pili kushoto,akizungumza na akinamama (hapo pichani) katika zahanati ya Mahina leo,wakati UWT Tawi la Mwananchi wilayani Nyamagana walipotembelea zahanati hiyo kugawa zawadi kwa watoto,wa kwanza kushoto ni Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo,Magembe Ng’walida.
Akinamama waliopeleka watoto wao kliniki katika zahanati ya Mahina wakimsikiliza Diwani wa Mahina (CCM) Alphonce Francis (hayupo pichani, leo alipoongozana na Mwenyekiti wa UWT Tawi la Mwananchi kugawa zawadi kwa watoto.
Mwenyekiti wa UWT Tawi la Mwananchi, Elizabert Magiri,leo akizungumzana akina mama katika zahanati ya Mahina (hawapo pichani),kushoto ni Katibu wa CCM Kata ya Mahina, Vitalis Makorosho na kulia ni Rose Leonard, Katibu wa UWT Mwananchi.
Akinamama wakimsikiliza Mwenyekiti wa UWT Tawi la Mahina,Elizabert Magiri,leo alipotembelea zahanati ya Mahina kugawa zawadi kwa watoto ambapo jumuiya hiyo ilikuwa ikiadhimisha miaka 47 ya kuzaliwa CCM.
Teddy Mugesi (kulia) akipokea kutoka kwa Diwani wa Mahina, Alphonce Francis, kwa niaba ya akinamama na watoto wao akipokea sabuni zilizotolewa zawadi kwa watoto hao leo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 47 ya CCM.
Lawrencia Machunda (kulia) kwa niaba ya akinamama na watoto wao akipokea boksi la vinywaji laini (juice) kutoka kwa Mwenyekiti wa UWT Tawi la Mwanza, zawadi hizo imetolewa na jumuiya hiyo ikiadhimisha miaka 47 ya CCM.
Mganga Mfawidhi wa Aahanati ya Mahina, Magembe Ng’walida (kulia) akitoa maaelezo kwa Mwenyekiti wa UWT Tawi la Mwananchi, Elizabert Magiri (katikati),Katibu Kata wa CCM Mahina, Vitalisi Makorosho (wa pili kushoto) na Diwani wa Mahina, Alphonce Francis, wa kwanza kushoto leo, walipotembelea wodi wazazi na cumba cha kujifungulia.(Picha na Baltazar Masha
…………
NA BALTAZAR MASHAKA,NYAMAGANA
JUMUIYA ya Umoja wa Wanawake (UWT) Tawi la Mwananchi wilayani Nyamagana,mkoani Mwanza,imeadhimisha miaka 47 ya CCM kwa zawadi kwa watoto na kuwaasa wanawake wakiwemo wanawaume kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya sita za kuboresha sekta ya afya.
Rai hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa UWT, Elizaberth Magiri, wakati akizungumza na akinamama katika zahanati ya Mahina ambapo walikabidhiwa zawadi mbalimbali za watoto zikiwemo sabuni.
“Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,ni mama mlezi wa jamii,tunapoadhimisha miaka 47 ya CCM tunajivuna amefanya makubwa ikiwemo kuboresha huduma za afya na huduma zingine zinazidi kusogea ili kuwasaidia akinamama,watoto na wazee,”amesema.
Elizabert amewataka wananchi wa Mahina kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu 2025,wajitokeze kushiriki na wanawake wasimsahau Rais Dk.Samia, wampe miaka mitano tena ili kumlipa fadhila kwa kazi kubwa aliyofanya ya maendeleo.
“Pia,ukimuelimisha mwanamke umeelimisha jamii yote,hivyo akina mama mfahamu madhara ya ugonjwa wa kipndupindu mkuchukue tahadhari zote na kujitahidi kuwa wasafi wa mazingira na watoto wasile vyakula bila kunawa,”amesema.
Kwa niaba ya akinamama wenzao,Prisca Benson aliishukuru UWT kwa zawadi za watoto pamoja na Rais Samia kwa kuboresha huduma za afya sasa wanapata huduma nzuri za matibabu zinazotolewa katika zahanati ya Mahina huku Rehema Daniel akiishukuru serikali kwa kuboresha huduma ya afya ya mama na mtoto.
Kwa upande wake Diwani wa Mahina (CCM),Alphonce Francis amempongeza Rais Dk.Samia kwa namna alivyomwaga fedha nyingi za miradi itakyowahudumia wananchi wa kata hiyo na kuwaomba wananchi waiunge mkono serikali katika eneo hilo la miradi.
Ameeleza huduma za afya zinazotolewa katika zahanati ya Mahina hazikidhi kulingana na idadi ya wananchi zaidi ya 50,000,ndio maana wanahitaji kituo kikubwa cha afya kwani azma ya serikali kila kata iwe na kituo cha afya.
“Tunataka wananchi na akinamama wafahamu nini serikali yao inafanya,tumepokea mradi wa jengo la upasuaji,litakapokamilika tunakwenda kutatua changamoto za afya wananchi wapate huduma nzuri karibu na jengo la wagonjwa wa nje (OPD) tayari limefikia asilimia 86 kukamilika na kuiwezesha Zahanati ya Mahina kuwa na hadhi ya kituo cha afya,”amesema.
Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo,Magembe Ng’walida amesema inahudumia wagonjwa 40 na wajawazito wanaojifungua 10 hadi 20 kwa siku, wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji hali inayozorotesha utoaji wa huduma,wanalazimika kununua ndoo ya maji kwa sh.500 nje ya bajeti wakati mahitaji ni ndoo 10 kwa siku.
Amesema jengo la OPD linalojengwa na TASAF litasaidia wagonjwa na kurahisisha utoaji na upatikanaji wa huduma ambapo huduma zote zitapatikana eneo moja badala ya kumsafirisha mgonjwa eneo jingine ingawa wanakabiliwa na uhaba wa viti,meza na dawati la wagonjwa.